Habari

Yanga yafafanua msimamo wake wa kutovaa jezi za Vodacom


Katibu wa Baraza la wazee wa klabu ya Young Africans Sports Club, Mzee Ibrahim Akilimali ametoa ufafanuzi juu ya timu ya Yanga kutovaa jezi zenye nembo nyekundu ya mdhamini wa ligi kuu Tanzania bara kampuni ya simu ya Vodacom.

Akiongea na wandishi wa habari makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga/Jangwani, Mzee Akilimali amesema kamwe hawatakubali matakwa ya vodacom na TFF ya kuweka nembo yenye doa jekundu katika jezi za Yanga.

Ni afadhali hao TFF watufute katika ligi yao kama wataendelea kutulazimisha kuvaa jezi zenye nembo nyekundu, kwani tupo radhi kubaki kucheza michezo isiyodhaminiwa na Vodacom kama bao, ngumi, na mingineyo au hata kuhamia ligi ya visiwani Zanzibar ambako tutacheza bila vikwazo.

“Labda kwa wasiofahamhu historia, Yanga mwaka 1953 mbele ya aliyekua Gavana wa Tanganyika, Sir Edward Twinning ilikataa kuvaa jezi zenye madoa ya rangi nyekundu ilizoletewa na timu pinzani ya mabaharia kutoka Uingereza, na kusema ni bora tucheze vifua wazi kuliko kuvaa jezi hizo,” alisema Mzee Akilimali.

Mzee Akilimali aliongeza pia kuwa hata chama cha TANU kiliwahi kuiomba Yanga ibadilishe rangi zake za kijani na njano, lakini Rais wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa Julius Nyerere aliwambia wajumbe wa TANU kwamba waacheni Yanga na rangi zao, rangi hizo wanazotumia zinawatambulisha wao, madini, na maliasili ya nchi hii.

Aidha pia Mzee Akilimali alisema mnamo mwaka 1963, aliyekuwa mkuu wa mkoa Dar es salaam mh Mustapha Songambele aliziita timu zote zilizokuwa na majina ya kigeni kwamba zibadilsihe majina hayo na kujiita majina ya kitanzania, timu zote zilibadilisha majina lakini Young Africans ilipotafsiriwa ilileta maana ya Vijana wa Afrika hali iliypolekea Yanga kuendelea kutumia jina lake, na timu zingine kubadilisha majina yao.

Kaimu katibu mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako amesema wanashindwa kuelewa kwa nini vodacom mwaka huu wanalazimisha Yanga ivae jezi zenye rangi jekundu, ili hali mwaka jana walikubali kutoa jezi zenye rangi nyeusi ya doa la vodacom.

“Mkataba kati ya TFF na Vodacom sisi hatujauona, sasa inakuwa vigumu kujua kipi kimeandikwa ndani ya huo mkataba na kinapaswa kutekelezwa, ilipaswa vilabu tuepewe nakala ya mkataba tuusome kabla ya kusainiwa, ili na sisi tupate nafasi ya kutoa hoja katika mkataba huo, lakini wao wamefanya kinyume kisha wanatulazimisha tuvae hiyo nembo, ikiwa hatujui maslahi ya mkataba wenyewe,” alisema Mwalusako.

Yanga itashuka dimbani siku ya jumamosi kucheza na timu ya Ruvu Shooting katika muendelezo wa michezo ya Ligi ya Kuu ya Vodaco nchini raundi ya 8.

Naye Mzee Mwika aliongezea kwa kutoa mfano kwamba “haiwezekani Mnyamwezi aje zake Pwani toka Tabora atukataze wazaramo kucheza mdundiko au dogoli”, alichokikuta anapaswa kukifuata na kukiheshimu na sio kuja na kutaka kubadillisha tamaduni za watu, Yanga ina rangi kuu tatu (3) Kijani, Njano na Nyeusi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents