Habari

Waziri mkuu akabidhiwa kazi ya kupambana na dawa za kulevya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kazi ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya akiwa kama Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Dawa hizo nchini.

Rais Magufuli ameyasema hayo Jumapili hii Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Peter Makakala, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Sianga pamoja na mabalozi watatu Mhe. Omary Yusuph Mzee, Mhe.Joseph Edward Sokoine pamoja na Mhe. Grace Aron Mgovano aliowateua hivi karibuni.

Dkt. Magufuli amesema kuwa Waziri Mkuu anatajwa kwenye Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ambapo Wajumbe wake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

“Nalipongeza sana Bunge la kipindi cha mwaka 2010 – 2015 chini ya Spika mstaafu, Mhe. Anne Makinda lililopitisha Sheria hii baada ya kuona sheria za mwanzo za kupambana na dawa za kulevya hazina nguvu hivyo Wabunge wa wakati ule walisimama kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao wakapitisha sheria hii,” alisema Dkt. Magufuli.

“Sheria imeeleza wazi katika kifungu cha 10 cha Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya linasimamiwa na Serikali pekee yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya au mtu yoyote atakayekuwa amepewa mamlaka ya kusimamia Serikali.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Taifa limeendelea kushuhudia kizazi kikiendelea kudidimia kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya na Serikali kwa mipango yake imeendelea kukemea, kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa hizo.

“Jambo hili limeleta athari kubwa sana kwani vijana wetu wengi wamepoteza uwezo wa kujisimamia katika shughuli zao za maendeleo kwa sababu baada ya matumizi tumeona athari kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa kwa mwili, uwezo wa kutafakari pamoja na kutoweka kwa uwezo wa kufanya kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Taifa hili la Watanzania kwa kiasi kikubwa linawategemea vijana waweze kuleta msukumo wa maendeleo ndani ya nchi hivyo jambo hili likiachiwa linaweza kuleta athari kubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo yetu kwa ujumla wake.

Alisisitiza kuwa vita hii ilianza, inaendelea na itaendelea kupiganwa hadi imalizike hivyo Watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada zozote zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi yake kwa namna yoyote ile, kila mmoja anatakiwa kushiriki kikamilifu ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ndani ya nchi hii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents