Habari

Watanzania wanaoishi nje waaswa kutojihusisha na biashara ya dawa za kulevya

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika na kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatano hii wakati akizungumza na Umoja wa Watanzania wanaoishi nchini Mauritius katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya Meridien mjini Port Louis.

“Vita ya dawa za kulevya ni kubwa, hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya. Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” amesema.

Amesema katika kudhibiti biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo, uwezo na mamlaka aliyonayo,”.

Aidha alisema mamlaka hiyo inafanyakazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo likiwa ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.

Katika hatua nyinngine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya Taifa.

Hata hivyo alisema ni vema wakatumia fursa walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na utalii.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed amewaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa umoja wao ndiyo nguzo yao.

“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie kilichowaleta,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni Ofisa wa benki ya Standard Chaetered nchini Mauritius amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.

Waziri Majaliwa alisema wanaunga mkono na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents