Bongo5 MakalaBurudani

Watanzania tusiwe mabingwa wa kuwabeza na kuwavunja moyo wasanii wetu (The Lupela Story)

Hivi ni chuo gani hicho kinachotoa shahada ya kubeza na kuvunja moyo wasanii? Inaonekana ni chuo kinachozalisha wahitimu wengi sana kila mwaka. Wahitimu hawa hutumia shahada yao Instagram, Youtube na Facebook kubeza kazi za wasanii wa nchi yao. Ni vigumu sana kuwaridhisha watu hawa, hata ufanyeje.

Kwanini nimeanza na maelezo hayo? Lengo kubwa hasa ni kuzungumzia jinsi ambavyo wahitimu wa shahada hiyo wanavyoizungumzia video ya wimbo mpya wa Alikiba ‘Lupela.’ Wanadai kuwa ni mbovu, mbaya, Kiba kachemsha na huku baadhi ya mashabiki wake mwenyewe wanadai amewaangusha. Nawapa pole sana kwa kutarajia vilivyozoeleka.

Hoja zao zinatofautiana, wapo wanaosema kwanini amevaa nguo ile ile kwenye video nzima, rangi yake sio nzuri, wengine wanasema haina hadhi ya kufanyika Marekani nk.

Katiba inawaruhusu kutoa maoni yao lakini wakati mwingine kuna tofauti kati ya maoni na kubeza. Mtu anayetoa maoni huangalia pande zote mbili za shilingi. Huanza kwanza kwa kuangalia mazuri aliyoyaona na kisha kukosoa kile anachoona hakijakaa poa. Au hukosoa na kisha hupongeza kwa mazuri aliyoyaona.

Nakubali kuwa Lupela sio video bora kuliko zote duniani na hivyo haiwezi kupendwa na kila mtu lakini kuna namna ya kuikosoa katika mtindo ambao msanii hatovunjika moyo na kuhisi kuwa amepoteza muda, nguvu na fedha kwa kazi yake.
Watu wanaobeza huwa na maneno mafupi yasiyo na hoja. Husema tu ‘mbaya’, ‘mbovu’, ‘kachemka’ nk. Ukiwauliza video ya Lupela ina ubaya gani hawawezi kuwa na hoja za msingi, basi tu watasema mbaya. Lakini hata wale wenye hoja, wanazo nyepesi sana ambazo hawewezi kuzitetea kwa mifano halisi.

Watu hawa wanakosoa video hii kwa kufuata kile walichozea kukiona. Mademu wakali kwenye video waliovaa vichupi, scenes za vitandani, kwenye swimming pool, magari ya kifahari, maghorofa nk. Watu hawa wanaamini kuwa video nzuri ni ile msanii amebadilisha nguo mara kumi na video iwe na rangi zinazovutia machoni.

Lupela ni wimbo uliodhaminiwa na Wildaid, shirika linalofanya kampeni ya kuhamasisha kupambana na ujangili na kuwahimiza watu wasitumie bidhaa zitokanazo na wanyama kama tembo, vifaru na wanyama wengine ambalo Alikiba ni mmoja wa mabalozi wake.

Wildaid wamefikiria wameona kuwa si vizuri kumwambia Alikiba atunge wimbo uitwao ‘Tusiue Tembo’ nk, kwakuwa idea itakuwa ‘too boring’ na haitoweza kuburudisha. Waliona ni vyema Kiba akaimba wimbo wa kawaida kabisa ambapo wataweza kuingiza ‘concept’ ya wanyama kwenye video yake.

Kilichofanyika ni kwamba WildAid walitaka Kiba amuimbie na kucheza na Lupela kwenye mbuga ambayo wanyama watakuwa wanapita nyuma yao. Na ujumbe wake hapa ni kwamba tunaweza kupendana na kufurahia mapenzi yetu tukiwa tumezungukwa na wanyama. Wanyama wana upendo na sisi hatupaswi kuwaua ili kutengeneza bidhaa tunazozitumia kwenye maisha yetu. Kwa kufanya hivyo Wildaid wanafanikiwa kumtumia Alikiba kama balozi wao kufikisha ujumbe huo katika njia inayoburudisha zaidi kuliko kama angeimba wimbo wenye ujumbe wa moja kwa moja.

Pia ni vyema kukumbuka kuwa video hii imeongozwa na Kevin Donovan, mmoja wa waongozaji wakubwa wa filamu Hollywood aliyeongoza filamu iitwayo Tuxedo ya Jackie Chan na Jeniffer Love. Sasa sijui kama wanaosema ‘mbovu’ wanajua zaidi kumzidi. Kukosoa ni rahisi sana.

Lakini pia tunapaswa kutoa credit kwa uchezaji uliotumika kwenye video hii. Yule dada Mmarekani, Aliya Janell na wale wengine wawili wametisha sana. Hakuna ubishi kuwa video hii inakuwa miongoni mwa video zenye uchezaji unaovutia zaidi. Kupitia urembo wake na uchezaji wake ulioenda shule, Aliya ametia nakshi ya kuvutia kwenye video hii. Hiyo nguo aliyoivaa mashallah inaongeza mvuto zaidi wa kumwangalia akicheza.

Janell

Angalia pia wale wasichana wawili wanaocheza wakiwa na vinyago usoni mwao. Vile ni vinyago vilivyotengenezwa kama kichwa cha tembo na pembe zake vinavyotumika kubeba ujumbe pia wa kuwalinda tembo dhidi ya ujangili.

Janell 2

Zingatia pia jinsi Alikiba alivyoonesha uwezo mzuri wa kucheza kwenye video hii. Sishangai hasa kwakuwa uchezaji wote huo umeongozwa na Oththan Burnside, choreographer aliyewahi kufanya kazi na Chris Brown, Rihanna, Nicki Minaj, Justin Bieber, Ne-Yo na wengine.

Kwahiyo sio kitu sahihi kwa mtu tu kuangalia video hii na kuhitimisha kwa kusema ‘mbovu’ bila kugusia vitu hivyo. Kuna tofauti kubwa kati ya ‘kukosoa’ na ‘kubeza’ au ‘kuponda’ na pale tunapobeza tufahamu kuwa tunawavunja sana moyo wasanii wetu ambao wana mioyo kama yetu, hawana mioyo ya chuma.

Na kiukweli wakati mwingine tunapoangalia video kiushabiki, tunajikuta tukiangalia zaidi kutafuta kosa kuliko kufurahia tunachokiona mbele.

Ukiangalia kwa ushabiki, mabaya ambayo ni machache, huyafunika mazuri ambayo ni mengi na kujikuta tukiropoka ‘mbovu.’ Pia tuziangalie video kwa upekee wake na sio kutaka kulinganisha na za wasanii wengine kuangalia ‘mbona huyu kafanya hivi, wewe umefanya vile?’ Kama kila msanii atafanya kitu kile kile, fikiria tutakuwa na industry inayoboa kiasi gani!

Muziki ni kitu kipana na kila mtu ana namna yake ya kuuwasilisha. Mapungufu yakiwemo tuyaseme kwa hoja za msingi ili kumjenga msanii na sio kwa kumbeza na kumvunja moyo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents