Habari

Watanzania 58 watimuliwa Msumbiji, wanyang’anywa mali na vitambulisho

Raia 58 wa Tanzania waliokuwa wanaishi nchini Msumbiji wamefukuzwa nchini humo na kurudishwa Tanzania huku wakidai kunyang’anywa mali zao, vitambulisho pamoja na hati za kusafiria na askari wa Msumbuji pasipo kujua sababu.

Raia hao watanzania ambao wamefukuzwa nchini Msumbiji wamesema wameacha mali zao, fedha walizokuwa nazo mifukoni wameporwa na askari wa Msumbiji wakati wanakamatwa. Wamedai sehemu zao za biashara ambazo walikuwa wamefungua wameziacha wazi. Bila kufuata taratibu raia hao waliwekwa mahabusu na baada ya siku tatu wakafikishwa kwenye mpaka Tanzania na Msumbiji, Kilambo mkoani Mtwara.

Miongoni mwa watanzania hao ni Ambali Ausi, Martida Mwakipesile, Mikidadi Abdallah, na Sakoma Mayamba walisema walikamatwa na kupakiwa kwenye gari na kuvushwa katika kivuko cha Kilambo, Mtwara.

Aidha mmoja kati ya watanzania waliofukuzwa aliyejulikana kwa jina la Mwakipesile alisema kuwa alikuwa ni mfanyabiashara wa chakula.

“Tulipakiwa kwenye lori na kupelelekwa kwenye kituo cha polisi cha Mtepweshi na kuwekwa ndani kwa siku tatu bila hata kula kitu chochote nikiwa na watoto wangu. Simu zetu pamoja na fedha zote walichukua, tunaiomba serikali itusaidie kutokana na unyama ambao tumefanyiwa,” alisema.

Kwa upande wake Abdallah ambaye ni mmoja waliofukuzwa pia alisema, “Hadi sasa bado hatujaelewa tatizo ni kitu gani kwa sababu asubuhi nimeamka na kwenda dukani kwangu nifungue, lakini nikakutana na askari nikafungwa pingu mkononi, nilipouliza nikajibiwa hakuna kuuliza, nikapelekwa kituoni tukafungiwa ndani kisha tukavushwa kurudi huku Tanzania.

Naibu kamishina wa uhamiaji ambaye ni afisa uhamiaji wa mkoa wa Mtwara Rose Mhagama anasema kitendo hicho kinatoa taswira mbaya kati ya nchi hizi mbili za Tanzania na Msumbiji licha ya kuwa na uhusiano mzuri na ujirani mwema.

By: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents