Habari

Wanakijiji wafukua, wala mizoga ya RVF

WAKATI ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF), ukitikisa mkoani hapa, baadhi ya wananchi wamekuwa wakifukua mizoga ya ng’ombe waliokufa kwa ugonjwa huo na kula, hali inayoongeza maambukizi.

Martha Mtangoo, Dodoma

 

WAKATI ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF), ukitikisa mkoani hapa, baadhi ya wananchi wamekuwa wakifukua mizoga ya ng’ombe waliokufa kwa ugonjwa huo na kula, hali inayoongeza maambukizi.

 

Katika tukio la hivi karibuni katika kata ya Huzi, Wilaya ya Chamwino mkoani hapa, wanakijiji walifukua mzoga wa ng’ombe aliyekufa na kufukiwa akihisiwa kukumbwa na RVF, wakagawana nyama na kula.

 

Tukio hilo lilitokea juzi usiku kwa wananchi wasiojulikana kufukua mzoga wa ng’ombe huyo na kula nyama kutokana na imani yao kuwa ng’ombe huwa hawazikwi wanapokufa.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mpwayungu, Haji Semniga, alisema alipata taarifa hizo juzi kuwa baadhi ya wananchi wa kata ya jirani ya Huzi walifukua ng’ombe aliyekufa kwa Homa ya Bonde la Ufa na kula.

 

Semniga alisema ng’ombe huyo alipokufa alichimbiwa shimo na akafukiwa, lakini usiku watu wasiojulikana walifukua shimo hilo, wakatoa mzoga, wakauchinja na kugawana nyama kwa ajili ya kitoweo.

 

“Jamii za wafugaji hawaamini kama ng’ombe huwa wanazikwa, na hii ndiyo sababu walifukua mzoga na kuula kutokana na imani yao kuwa ng’ombe hazikwi kama binadamu,” alisema. Semniga alisema katika kata yake amepiga marufuku uchinjaji wa ng’ombe, lakini bado wananchi wanachinja, wanakula nyama ya kuchoma na kunywa maziwa ambayo hayajachemshwa.

 

Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Huzi, Wilson Mihinzo alisema wakati tukio hilo linatokea hakuwapo kijijini hapo. Hata hivyo taarifa za tukio hilo zimemshtua kwa kuwa limedhihirisha kuwa bado wananchi wa vijijini hawaelewi hatari ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa.

 

Mihinzo alieleza wasiwasi wake kuwa kutokana na hali hiyo wananchi wataendelea kufa kwa ugonjwa huo kwa kuwa bado wanaendelea kula nyama ya kuchoma na wengine wanachinja ng’ombe usiku kwa siri na kuuza bila kujua madhara yake. Alisema yeye kwa kushirikiana na diwani wa kata yake wamekwisha kufanya mikutano ya hadhara kuwatahadharisha wananchi hatari ya ugonjwa huo ingawa hayajaonekana mafanikio yoyote katika kata hiyo.

 

Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nkhambaku, Iyana Makulo aliwaomba mabwana afya kusaidia uhamasishaji wa wananchi kuhusiana na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa kwa kuwa wao kama maofisa watendaji hawana elimu wala utaalamu juu ya ugonjwa huo.

 

Wakati huo huo, maduka ya kuuzia nyama mjini Dodoma yamefungwa baada ya watu kuacha kula nyama kutokana na ugonjwa huo. Mwandishi wa habari hizi jana alishuhudia duka maarufu la kuuzia nyama la Mshikamano likigawa zaidi ya kilo 20 za nyama kwa baadhi ya watu na ombaomba baada ya nyama hiyo kukaa kwa muda mrefu katika jokofu bila kupata wateja.

 

Muuzaji wa nyama katika duka hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Halima, alisema kutokana na hali hiyo duka hilo litakuwa likiuza nyama ya kuku kwa vile kuku mmoja kwa sasa anauzwa kati ya Sh 5,000 hadi Sh 8,000, wakati awali kuku walikuwa wakiuzwa Sh 2,500 hadi Sh 3,000.

 

Maduka mengi kwa sasa yanauza samaki wabichi ambao kwa kilo ni kati ya Sh 4,000 hadi Sh 5,000. Awali walikuwa wakiuzwa Sh 2,500 kwa kilo. Wauzaji wa nyama ya nguruwe mjini hapa nao wako katika hali nzuri kwa vile wananchi wengi zaidi wanakula nyama hiyo baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, kutangaza kuwa hakuna uhakika kama nguruwe anaambukizwa ugonjwa huo.

 

Nyama ya nguruwe kwa sasa inauzwa Sh 2,500 kwa kilo na hapo awali ilikuwa ikiuzwa Sh 1,800 kwa kilo.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents