Siasa

Waliotangaza kumshitaki Dkt. Slaa wanywea

VIGOGO wa Serikali waliotajwa kwenye orodha ya tuhuma za ufisadi na kutishia kufungua kesi dhidi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, kwa walichokiita kuwakashifu, wako kimya mpaka sasa.

Na Reuben Kagaruki

 

VIGOGO wa Serikali waliotajwa kwenye orodha ya tuhuma za ufisadi na kutishia kufungua kesi dhidi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, kwa walichokiita kuwakashifu, wako kimya mpaka sasa.

 

Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata baada ya kufuatilia kwa takriban wiki mbili na kuthibitishwa na waliotishiwa kufunguliwa kesi na vigogo hao, akiwamo mwanasheria wa CHADEMA ambaye ni wakili wa kujitegemea, Bw. Tindu Lissu na uongozi wa gazeti la Mwana Halisi zimeeleza kuwa hadi sasa hakuna kesi iliyofunguliwa.

 

“Hakuna kesi iliyofunguliwa dhidi yetu, kama wangefungua kesi si wangetuita kutueleza hata kwa maandishi?,” alihoji Bw. Lissu alipozungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana.

 

Kauli kama hiyo ya Bw. Lissu pia ilitolewa na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwana Halisi, Bw. Saed Kubenea, ambaye alisema hawajapokea hati yoyote ya kuitwa mahakamani.

 

“Mtu anayelalamika ndiye anayepaswa kwenda mahakamani sisi hatujapata hati yoyote ya kuitwa,” alisema Bw. Kubenea.

 

Gazeti hilo lilitishiwa kufunguliwa kesi na vigogo hao kwa madai ya kuchapisha na kusambaza habari zilizowatuhumu kwa ufisadi.

 

Takribani miezi minne iliyopita katika mkutano wa hadhara uliitishwa na umoja wa vyama vinne vya upinzani katika viwanja vya Mwembe Yanga, Dar es Salaam, Dkt. Slaa alitaja orodha ya vigogo 11 akiwahusisha na ufisadi.

 

Baadhi ya vigogo ambao walitajwa kwenye orodha hiyo na kutishia kwenda mahakamani iwapo hawataombwa radhi na kulipwa fidia ni Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bw. Gray Mgonja.

 

Mwingine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bw. Patrick Rutabanzibwa, ambaye pia alitaka aombwe radhi, vinginevyo aende mahakamani.

 

Mtuhumiwa mwingine, mwanasheria mkongwe, Bw. Nimrod Mkono, alishasema hana haja ya kwenda mahakamani kwani Dkt. Slaa, hana fedha za kumlipa fidia.

 

Pamoja na kuandikiwa barua ya mawakili wa Bw. Karamagi wakimtaka Bw. Lissu kumwomba radhi na kumlipa fidia ya sh. bilioni 10, alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema kama Waziri Karamagi anataka kwenda mahakamani aende “lakini itabidi aithibitishie uadilifu alionao anaotaka ulindwe na mahakama.”

 

Hivi karibuni, baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daud Balali, vyombo vya habari vilimkariri Dkt. Slaa akihoji Serikali kutowachukulia hatua vigogo aliowataja katika ‘orodha ya mafisadi’.

 

“Orodha ya mafisadi imeishia wapi, wananchi wanataka kujua hawa watachukuliwa hatua lini, wengi walitishia kwamba watanipeleka mahakamani, lakini hakuna hata mmoja aliyethubutu kufanya hivyo,” alisema Dkt. Slaa.

 

Gazeti hili lilipofuatilia kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ili kujua kama vigogo hao wamefungua kesi juhudi hizo zilishindikana kwa kilichodaiwa ni wahusika kuwa likizo.

 

Tangazo lililobandikwa katika ubao wa matangazo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam lilieleza kuwa Mahakama Kuu na ya Rufaa nchini zimefungwa kuanzia Desemba 15 mwaka jana hadi Februari 4 mwaka huu kutokana na watumishi wa mahakama hizo kwenda likizo ya kawaida.

 

Kesi na shughuli nyingine za mahakama hizo zitaendelea kama zilivyopangwa kuanzia Februari 4. Hata hivyo chanzo chetu kutoka ndani ya mahakama hiyo, kilieleza kuwa hadi wanakwenda likizo, hakuna kesi iliyokuwa imefunguliwa ya vigogo hao.

 

Waziri Karamagi alipopigiwa simu yake ya mkononi jana ili aeleze sababu za kuchelewa kufungua kesi kama alivyotangaza, alisema yuko kwenye ziara ya Rais Kikwete mkoani Kagera, hivyo hakuwa katika nafasi ya kulizungumzia.

 

“Hapa niko katika ziara ya Rais, subirini nikirudi Dar es Salaam ndipo mniulize hilo,” alisema Bw. Karamagi.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents