Habari

Wakurugenzi halmashauri waishambulia PCB

WAKATI Serikali imekuwa ikilalamikia kushamiri kwa rushwa katika halmashauri nchini, Mameya na Wakurugenzi wa halmashauri hizo wameichachamalia Taasisi ya Kuzuia Rushwa Tanzania (PCB)

Oscar Mbuza


WAKATI Serikali imekuwa ikilalamikia kushamiri kwa rushwa katika halmashauri nchini, Mameya na Wakurugenzi wa halmashauri hizo wameichachamalia Taasisi ya Kuzuia Rushwa Tanzania (PCB), wakidai kwamba haina uwezo wa kupambana na rushwa kubwa zinazoathiri uchumi wa nchi.


Wakizungumza kwenye warsha ya kujadili Muswada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 inayowahusisha wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na maofisa wa PCB, Dar es Salaam jana, Mameya na Wakurugenzi hao walisema PCB imekuwa ikihangaika zaidi na rushwa ndogo ndogo.


“Hatuna imani na uwezo wa PCB, haina uwezo wa kupambana na rushwa kama ya rada ambayo kwa kweli ni uhujumu wa uchumi wa taifa letu, badala yake PCB inahangaika na rushwa ndogo,” alisema Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Hassan Mwendapole.


Alisema PCB imejikita zaidi kwenye rushwa ambayo madhara yake yanaonekana kwa urahisi na kushindwa kupambana na rushwa ambayo madhara yake yanaonekana baadaye wakati yakiwa tayari yamesababisha athari kubwa kwenye uchumi wa Taifa. “PCB inapambana na rushwa kwenye huduma, lakini imeshindwa kupambana na rushwa kwenye uchumi wa nchi, hata kwa sheria mpya hakuna lolote litakalofanyika,” alisema Mwendapole.


Meya wa Jiji la Mbeya, Atanas Kapunga, alisema tangu kuanza kutumika kwa Sheria ya Rushwa namba 16 ya mwaka 1971, PCB imekuwa ikiwakamata wala rushwa wadogo wadogo, lakini imeshindwa kufanya hivyo kwa wala rushwa wakubwa serikalini.


Meya wa Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo alisema vigogo wa Serikali wamekuwa wajanja wa kutumia upungufu wa sheria na Mahakama kukwepa kutiwa hatiani kwa kuhusika na rushwa.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents