Habari

Wajasiriamali wa kike Dodoma walalamika kuombwa ‘uroda’ ili wapewe vibanda vya biashara

Serikali mkoani Dodoma imeombwa kuingilia kati mgogoro katika soko lisilo rasmi la Rehema Nchimbi kutokana na malalamiko ya wajasiriamali wanawake kuombwa rushwa ya ngono sambamba na kulipishwa fedha bila kupewa risiti.

Walitoa malalamiko yao juzi mbele ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya uongozi wa soko hilo kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano ambao ulikuwa ufanyike siku hiyo hautakuwepo, jambo ambalo lilikataliwa na wajasiriamali hao.

Mmoja wa wajasiriamali katika soko hilo, Prisca Chibwaye alisema baadhi ya viongozi wa soko wanatumia nafasi zao kuwanyanyasa wanawake kwa kuwaomba rushwa ya ngono, huku wakilipishwa fedha bila kutoa risiti kwa madai kuwa malipo hayo ni kwa ajili ya kuchangia ukarabati wa soko hilo.

Alisema viongozi hao wamekuwa ni kero kubwa hususani kwa wanawake ambao wamekuwa wakidaiwa michango na hata rushwa ya ngono kila mara.

“Wakati mwingine wanatunyanyasa hata kututishia kutunyang’anya mabanda yetu ukizingatia kuwa tulio wengi tumekodi,” alisema.

Mjasiriamali mwingine, Mwajuma Rashidi, alisema uongozi huo wa soko umekuwa kero kwao kutokana na kufanya mambo yao bila kushirikisha wafanyabiashara na haujawahi kuitisha mkutano hata moja tangu ulipoingia madarakani zaidi ya miaka sita sasa.

Alisema wamekuwa wakikabiliawa na changamoto kubwa ya kuombwa rushwa ya ngono kutoka kwa baadhi ya viongozi na suala hilo liangaliwe kwa makini ili ufumbuzi wake uweze kupatikana. Alisema kuna wakati dada mmoja aliwahi kuomba kukodishwa banda kwa ajili ya biashara na akaombwa rushwa ya ngono ambayo aliitoa.

“Kwa bahati mbaya dada huyo akapata mgonjwa akaenda kumuuguza aliporudi akakuta banda kapewa mtu mwingine tena anaombwa atoe rushwa ya ngono ili aweze kupatiwa jingine.Sasa tutakua tunatoa ngono kila siku hadi tupate mimba?” alihoji.

Mwenyekiti wa soko hilo, Norbert Pangasero akijibu madai ya wafanyabiashara hao alikiri kuyapokea malalamiko hayo na kudai kuwa wanatarajia kuitisha mkutano ndani ya wiki hii ili kusikiliza kero zote.

BY: Emmy Mwaipopo

Chanzo:Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents