Wabunifu chipukizi wapatikana
Wabunifu 8 wenye vipaji wameingia katika fainali za kushindania zawadi za maonyesho makubwa ya mavazi ya Swahili Fashion Week 2010 wamepatikana.
Uchaguzi huo wa wabunifu wa mavazi wanaochipukia ulifanyika Jumapili katika Hoteli ya Southern Sun Hoteli jijini Dar es Salaam, ambapo majina 8 yaliteuliwa na jopo la majaji wanne ambao ni Nsao ShaluA, Mkurugenzi wa sanaa kutoka baraza la sanaa la Taifa (National arts Council), Jamila Swai, mbunifu wa mavazi wa hapa nchini, Michelangelo Adam kutoka Ubalozi wa Italia hapa nchini pamoja na Mustafa Hassanali, kati ya waratibu wa Swahili Fashion Week 2010.
Wabunifu hao waliobahatika kuingia fainali, watashindana kwa kuonyesha kazi zao katika maonyesho makubwa ya wiki ya mavazi ya Swahili fashion week itakayofanyika Novemba mwaka huu.
Wabunifu wa mavazi wanaochipukia waliofanikiwa kuingia fainali ni pamoja na Narendrakumar Jeshang, Abdul Urassa, Shaban Wahure, Angelina Muna na Grace Kijo.
Awali mratibu wa Swahili Fashion Week,Washingtone Benbella alisema kuwa wabunifu wote 16 walikuwa wazuri na wameonyesha vipaji vya hali ya juu, na kuonyesha kuwa Tanzani ina vipaji vikubwa katika sanaa ya ubunifu wa mavazi.
Ni mara ya tatu tangu Swahili fashion week kuanzishwa na inatarajiwa kufanyika tena Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.