Habari

Viongozi wa umma 100 matatani

Viongovi wa umma wapatao 100 wameshindwa kuwasilisha tamko la rasilimali, maslahi na madeni yao katika Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma hadi kufikia Oktoba 30, mwaka huu.
waziri-kipacha
Katibu anayeshughulikia Viongozi wa Siasa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipach

Idadi hiyo ni kati ya viongozi wa umma 15,624, wanaowajibika chini ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Idadi hiyo ilitamkwa na Katibu anayeshughulikia Viongozi wa Siasa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha, wakati akizungumza na gazeti hili katika Chuo cha Maofisa wa Polisi, Kidatu, mkoani Morogoro juzi.

Chuo hicho kinaendesha mafunzo ya wiki mbili ya uchunguzi na mbinu za uendeshaji mashauri kwa Maofisa Uchunguzi na Maafisa Sheria wapatao 39 wa sekretarieti hiyo.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo ambaye naye kwa nafasi yake, aliwataka maofisa uchunguzi na maofisa sheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuhakikisha mali na madeni ya viongozi wa umma, zinahakikiwa ipasavyo na wote ambao wataonekana kudanganya, wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Pamoja na kutoa kauli ya idadi ya vigogo ambao hawajafikisha matakwa ya sheria, Kipacha alitaka viongozi hao kuwasilisha haraka matamko hayo. Alisema ingawa kuna watumishi hao 100 ambao hawajawasilisha matamko yao, zoezi hilo la kisheria limefanyika kwa mafanikio makubwa.

Ilomo pia aliwataka maofisa uchunguzi na maofisa wa sheria, kutekeleza majukumu yao kwa haki na kutanguliza maslahi ya umma. Pia aliwataka kufanya uchunguzi kwa kiongozi yeyote, anayeonekana kuvunja maadili ya uongozi.

Alisema ni matarajio ya umma kwamba kazi zao, zitawezesha kupungua kwa vitendo vya uovu wa maadili ndani ya Serikali na Utumishi wa Umma; na hivyo kujenga na kudumisha misingi ya utawala bora na kukuza uadilifu miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma.

Katibu anayeshughulikia viongozi wa umma, John Kaole, alisema mafunzo hayo yataendeshwa kwa awamu mbili kwa maofisa 40 kila awamu, yakilenga uhakiki wa mali na madeni, mbinu za kuthaminisha rasilimali na uchunguzi katika sekta ya umma, utakatishaji wa fedha, uchunguzi na ukaguzi wa taarifa za fedha, mbinu za uendeshaji wa mashauri, uandaaji wa hati za kisheria na maadili ya uchunguzi.

Pia marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995, yaliyofanyika hivi karibuni. Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maofisa wa Polisi Kidatu, Andrew Mwang’onda alisema mafunzo hayo yatawasaidia maofisa hao na wachunguzi, kujenga upya maadili ndani ya jamii, ambayo tayari yameanza kumomonyoka.

Source: Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents