Habari

Viongozi wa kijiji mbaroni kwa tuhuma za kujinufaisha na shilingi milioni 5 za TASAF

Polisi wilayani Kalambo imewakamata viongozi tisa wa serikali ya kijiji cha Serengoma wilayani humo kwa tuhuma za kujinufaisha na shilingi milioni tano zilizolengwa kwa ajili ya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf III).

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven ametoa amri ya kukamatwa viongozi hao wakati yeye na wao wakiwa kwenye mkutano huku mkuu wa polisi wa wilaya akitekeleza amri hiyo na watuhumiwa kukamatwa muda huo huo.

Zelothe amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kuhakikisha watumishi wote wa umma waliosababisha matumizi mabaya ya fedha hizo kwa kuwaingiza wasiostahiki katika mpango huo, zikiwemo kaya hewa, wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Baada ya kusikiliza kero za wanufaika wa mpango huo, Zelothe alimwagiza Mkuu wa Polisi wilayani hapa kuwakamata viongozi hao tisa wa serikali ya kijiji cha Serengoma, wanaotuhumiwa kujinufaisha na fedha hizo huku akimpa Mkuu wa Wilaya siku moja ahakikishe watuhumiwa wote 50 wamekamatwa na washitakiwe mahakamani

Aidha amewataka wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za wilaya za Kalambo, Nkasi, Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga wahakikishe wataalamu wao wanawasaidia wanufaika wa mpango huo ili watumie fedha wanazopata kwa manufaa “Serikali haitasita kuwachukulia hatua watakaonda kinyume na utaratibu,” alisisitiza.

BY: Emmy Mwaipopo

Chanzo:Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents