Habari

Vigogo 5 jela miaka mitano kwa kula rushwa na utakatishaji wa fedha

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewakuta na hatia na kuwahukumu kifungo cha miaka 5 jela au kulipa faini ya Sh milioni 100 kila mmoja vigogo watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa na utakatishaji wa fedha.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dar es Salaam jana ilisema kesi hiyo iliyoendeshwa kwa muda mrefu na kufuatiliwa na watu wengi ilifunguliwa Julai 21, mwaka 2010.

Taarifa hiyo ya Takukuru iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wake Mussa Misalaba iliwataja washtakiwa waliopatikana na hatia kuwa ni Justice Lumina Katiti aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na Marcus Mussa Masila aliyekuwa Mhasibu wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL.

Wengine ni Kanuti Ferdinand Ndomba mfanyabiashara wa Kampuni ya UEE Tanzania Limited, Gidion Wasonga Otullo mfanyabiashara wa kampuni ya East Africa Procurement Services na Robert Phares Mbetwa mfanyabiashara kutoka kampuni ya Romos Technology Limited.

Kesi hii iliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na TAKUKURU ambao ni Awamu Mbagwa (DPP), Shedrack Kimaro (DPP), Estazia Wilson (DPP) na Marx Ally (Takukuru).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Takukuru, hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama hiyo Januari 17 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Renatus Rutatinisibwa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na hivyo kuwatia hatiani washtakiwa kwa jumla ya makosa 51 ya rushwa na utakatishaji wa fedha haramu.

Washtakiwa walipelekwa Magereza kutumikia kifungo cha miaka 5 baada ya kushindwa kulipwa faini hiyo ya Sh milioni 100.

Ilidaiwa kuwa kati ya mwaka 2007 na 2009 watuhumiwa kwa kushirikiana walikula njama kuchepusha Sh 3,399,251,740.24 za TTCL zilizokusudiwa kulipa kodi TRA na kulipwa kinyume cha sheria kampuni ya UEE. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Masila aligushi sahihi za watia sahihi wa TTCL na kubadili fomu za TIS zilizokusudiwa kupeleka fedha TRA na kuweka jina la UEE.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa Katiti alionesha kwenye mfumo wa TRA kuwa TTCL ilikuwa imelipa kodi zote. Ilidaiwa kuwa kati ya mwaka 2008 na 2009 Katiti , Masila, Wasonga na Mbetwa walijipatia mali nyingi na kununua magari ya kifahari na nyumba kutokana na fedha hizo haramu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents