Burudani

Video: Maamuzi ya rufaa ya Tigo dhidi ya hukumu ya kuwalipa AY na FA bilioni 2.18 kutolewa June 27

Mahakama Kuu ya Tanzania leo imesikiliza mapingamizi ya awali ya maombi ya rufaa yaliyowasilishwa na kampuni ya mawasiliano nchini Tigo dhidi ya hukumu iliyotolewa na mahakama ya wilaya ya Ilala, April 11 mwaka huu ya kutakiwa kuwalipa AY na Mwana FA shilingi bilioni 2.18 kama fidia ya kutumia nyimbo zao bila ridhaa yao.

Msando 3
AY akiwa na mwanasheria wake Alberto Msando nje ya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam

Mapingamizi hayo matatu yamewasilisishwa na Mwana FA na AY kupitia mwanasheria wao, Alberto Msando. Miaka minne nyuma, wasanii hao wawili walifungua kesi ya madai dhidi ya kampuni ya Tigo baada ya kutumia nyimbo zao ‘Dakika Moja’ na ‘Usije Mjini’ kama miito ya simu kwa wateja wake bila kuwa na mikataba nao.

Ijumaa hii, Mhe. Isaya Arufani ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania alisikiliza utetezi kutoka kwa mawakili wa pande hizo mbili. Mwana FA na AY walikuwepo pia mahakamani hapo.
Mhe. Arufani ametaija June 27 kuwa siku ya kusikilizwa kwa maamuzi ya Mahakama Kuu kuhusiana na rufaa hiyo.

Msando 1
Alberto Msando akizungumza na mwanasheria wa kampuni ya Law Associates inayoiwakilisha kampuni ya Tigo kwenye kesi hiyo

“Kilichokuwepo leo ni kusikilizwa kwa mapingamizi ya awali ya maombi waliyoleta Tigo ya kuomba kwamba kuzuia kukaza hukumu iliyotolewa na mahakama ya Ilala. Kwahiyo leo tumesikilizwa mapingamizi hayo na mahakama itatoa maamuzi yake tarehe 27 mwezi wa sita kuhusu mapingamizi ambayo tumeyaweka dhidi ya maombi yao,” Alberto Msando, mwanasheria anayewawakilisha AY na Mwana FA ameiambia Bongo5 mahakamani hapo.

“Yalikuwa mapingamizi matatu kwamba maombi yao yamekiuka baadhi ya vifungu vya sheria,” aliongeza Msando.

Msando 4
AY na Mwana FA wakiwa na mwasheria wao, Alberto Msando

Kwa upande wake Rosan Mbwambo wa kampuni ya Law Associates inayoiwakilisha Tigo kwenye kesi hiyo amedai kuwa kampuni hiyo haikuridhika na hukumu iliyotolewa na mahakama ya wilaya ya Ilala ndiyo maana imekata rufaa.

“Sheria inaruhusu ukishakata rufaa uombe hukumu isitekelezwe mpaka rufaa isikilizwe. Tigo wanasema tu wao hawajaridhika na kwasababu mfumo wa kimahakama unaruhusu mtu asiporidhika kwenda juu, wameenda juu tu kwa kuomba mahakama ya juu iangalie upya,” alisema Mbwambo.

Katika hukumu ya awali iliyotolewa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Ilala, Juma Hassan, Tigo walitakiwa kulipa shilingi milioni 25 zingine kama fidia kutokana na hasara waliyoipata wasanii hao kwa kutumiwa kwa nyimbo zao. Hiyo imekuwa hukumu kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwenye kesi zinazohusiana na haki miliki za kazi za muziki nchini Tanzania.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents