Bongo5 MakalaBurudani

Video kali ni dawa ya kukwepa geti gumu la promo za radio

Wewe ni msanii mpya? Umesharekodi wimbo wako na kuupeleka kwenye vituo vya redio? Jibu gani ulilolipata baada ya kuongea na DJ uliyekutana naye? Kama ni msanii uliyepitia yote hayo, jibu utakuwa nalo. Nina uhakika pia kwa wengi majibu yao yatakuwa yanafanana, kwamba majibu uliyoyapata mengi yalikuwa ya kukatisha tamaa.

yeezus-new-cover

Shughuli ya kusambaza wimbo wako kwenye vituo vya redio ni ngumu sana hasa kwa wasanii wachanga wasio na connection yeyote. Kwakuwa nimeshawahi kuwa mtangazaji na ninakumbuka jinsi ambavyo walinzi walikuwa wakiniita ofisini na kuniambia nina mgeni getini anayehitaji kuniona, mara nyingi wageni wangu walikuwa wasanii wachanga waliokuwa wakileta CD zao na nyingi zilikuwa hazivutii machoni hasa kwakuwa zilikuwa zimechafuka kwa kuandikwa vibaya na mark pen.

Ilikuwa ni ngumu kushawishika kuwa, wimbo uliomo kwenye CD hiyo ulikuwa mkali na unastahili dakika zangu 4 za kukaa na kusikiliza. Ukweli ni kwamba, nyimbo nyingi za aina hiyo zilikuwa mbovu, hazina kiwango cha kuchezwa kwenye redio kutokana na utayarishaji mbaya na makosa mengi yasiyovumilika.

Mara nyingi hali hiyo ilinifanya niwe mgumu wa kutilia maanani nyimbo nyingi za wasanii wachanga na wasiojulikana kabisa, na hivyo kuwaathiri wasanii wengine waliokuwa na nyimbo nzuri. Hii ni kwasababu CD nyingi nilijikuta nakosa mzuka wa kuzisikiliza na hivyo kuziweka tu kwenye kabati la studio, na zikiwa nyingi basi nazitupa kapuni.

Digital-Discs-In-Dustbin

Hicho ndicho kimekuwa kikiwatokea wasanii wengi wanapopeleka CD zao kwenye vituo vya redio. Wanaoweza kupata nafuu ni wale waliorekodi kwenye studio za maproducer wanaofahamika. Msanii mchanga aliyerekodi wimbo wake kwa Marco Chali, Lamar ama kwa P-Funk hawezi kupokelewa sawa na yule aliyerekodi kwenye studio changa ya Tandale iliyochini ya producer asiye na jina kabisa.

Mara nyingi madj huamini producer kama Majani hawezi kutengeneza wimbo mbovu na hivyo huwa na imani zaidi na nyimbo zinazotoka kwa maproducer wenye majina.

Nature ya upigwaji wa nyimbo kwenye vituo vingi vya redio nchini inafanana. Nyimbo zinazopigwa ni za wasanii wanaojulikana zaidi. Za wale wachanga hupigwa kwa sababu, aidha ni kali sana, wasanii wenyewe wana connection nzuri na madj ama kama wamempa mtangazaji mkwanja wa maji. Hiyo inaitwa ‘hela ya promo’.

Na by the way, hicho si kitu kinachofanyika Tanzania peke yake kama wengi wanavyodhani. Hata Marekani ambako tumekuwa tukipatumia kama mfano bora wa jinsi kiwanda cha muziki kinatakiwa kuwa, record labels hutenga bajeti kubwa kwaajili ya kufanya promotion ya nyimbo za wasanii wao kwakuwa bila kufanya hivyo, nyimbo huishia kuchezwa kwa siku chache tu na kupotea kabisa.

Hivyo, kwa wasanii wengi, kutokana na ukweli kwamba nyimbo mpya zinatoka kila siku, promo imekuwa ngumu sana hasa kwa redio kubwa zinazotegemewa zaidi. Hata wasanii wakongwe nao wamejikuta wakilalamika kwa kukosa promo na kulifanya tatizo hili kuwa kubwa kwa karibu robo tatu ya wasanii nchini.

Hata hivyo, mambo hayako hivyo kwenye vituo vya runinga. Bado TV zina nafasi nzuri zaidi kwa kutoa promo kwa video bila gharama ama usumbufu kama ilivyo kwenye redio.

Ni video ngapi ambazo umekuwa ukiziona kila siku kwenye TV, lakini hujawahi kusikia wimbo huo ukipigwa kwenye redio? Ni nyingi bila shaka. Hiyo ni kwasababu hakuna ushindani mkubwa kwenye TV kama ilivyo kwenye redio. Wasanii wajanja wameligundua hilo na sasa wamekuwa wakielekeza nguvu zaidi kwa kufanya video kali. Kuna njia nyingi za kufanya. Moja kubwa inayotumika zaidi ni kuachia wimbo wako kwenye radio na kisha fanya video yake.

Hakikisha video inakuwa nzuri kuendana na uzuri wa wimbo wako. Hii ni kwasababu, kama utafanya video nzuri, itatumika kama ‘booster’ ya wimbo wako na kuwashawishi madj wengi kuucheza bila hata kuhangaika sana kuomba promo.
Njia ya pili ni kuachia vyote kwa pamoja, yaani wimbo na video kama alivyofanya Diamond Platnumz kwenye My Number 1. Kama video ni kali na kutokana na urahisi wa video kuchezwa kwenye TV, watangazaji ama madj watajikuta wakitaka kuucheza wimbo huo wao wenyewe au kutokana na kuombwa na wasikilizaji waupige kwaajili yao.

Njia ya tatu ni kwa kuachia video peke yake. Kama video ni kali na ikawa inachezwa mara kwa mara, kutatengeneza hitaji lisiloepukika la wimbo huo kutakiwa kuchezwa kwenye redio na hivyo itakurahisishia wewe pale utakapoamua kuusambaza kwakuwa watangazaji na madj wengi watakuwa wanaufahamu kutokana na video yake.

Hivyo katika kipindi hiki ambapo promo ya wimbo imekuwa ngumu, ni muhimu wasanii wakawekeza zaidi katika kufanya video bora za nyimbo zao kuliko kubaki wakihangaika na promo ya radio zinazowaumiza vichwa wasanii wengi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents