Habari

Uzalendo sio kutoongea Kiingereza bali kuchukia maovu na ujinga ndani ya nchi yako

Baba wa taifa alisema tuna maadui watatu wakubwa ambao ni Umaskini, Maradhi na Ujinga. Mara nyingi umaskini na maradhi huletwa na ujinga wa watu wenyewe, hivyo kutokana na ujinga huo watu tumekuwa na mitizamo ambayo si sahihi kwetu wenyewe na kwa watu wengine kwa kuhusisha vitu visivyohusiana kabisa kwa sababu tu ya ujinga wetu.

Boy-Say-Do-you-speak-English

Tuna tatizo kubwa la ujinga ambao umetia giza fahamu na akili zetu kiasi kwamba hatujui ni nini maana ya kuwa mzalendo hivyo kuwaona wale ambao labda wanaongea Kiingereza ndani ya nchi yetu si wazalendo, na wale wanaojua kuongea Kiswahili wanaonekana ni wazalendo na kujivuna kwa hilo.

Wanawezekana wakawa sahihi au si sahihi.

Leo ninakupa changamoto ambayo tunatakiwa kuibeba kama watanzania na vijana wa nchi hii katika usemi usemao ‘Samaki mkunje angali mbichi’

Leo nilipokuwa nikisoma maana ya uzalendo, nimekutana na maneno kama kuipenda nchi yako na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya nchi yako katika kufanya mazuri kwa ajili ya nchi yako. Hivyo unatakiwa ujue kama kweli wewe unaipenda nchi yako na uko tayari kujitoa kwa ajili ya nchi yako kama unajua Kiingereza au hujui, kama unajua Kiswahili au hujui kama unajua lugha tu ya kwenu hujui Kiswahili au Kiingereza ilimradi ni raia wa nchi husika huwezi kukwepa kuwa mzalendo wa nchi hiyo.

Kuna vitu vya msingi ambavyo vinakusaidia kujumuika na watu wengine. Lugha ni kiungo cha msingi sana kujua na kutofautisha huyu mtu anatokea jamii fulani lakini si kipimo cha uzalendo wa mtu huyo katika jamii husika, kwakuwa unaweza kuwa mtanzania unaongea Kiswahili kizuri zaidi lakini huipendi nchi yako. Ujinga tulionao ni kuhusisha vitu visivyo vya msingi sana kuvifanya vya msingi na kusahau msingi tulionao kama watanzania kuwa ni upendo, amani na Utulivu.

Ninachotaka kusema tunahitaji watanzania wanaojua kuongea lugha ya Kiswahili, Kiingereza hata na Kifaransa au kichina n.k kwa sababu tunapata shida katika mawasiliano na namna ya kuwasiliana na watu wengine katika nyanja mbali mbali hasa tunapoingia kwenye taaluma, biashara.

Nimekuwa nikipata habari nyingi sana kwa wale ambao wanafanya kazi hasa kwenye taasisi za kimataifa, watu wetu wanajua kufanya kazi vizuri ila inapokuja suala la kuelezea wanachokifanya kwa lugha tofauti na Kiswahili utatamani ujifiche uvunguni.

Suala ni moja tu, tuondoe ujinga tulioweka ndani ya akili zetu na tujifunze umuhimu wa kujua namna ya kuwasiliana na wenzetu wa lugha yetu na wengine wa lugha nyingine ingawa kuna wengine watasema tunatakiwa kujivunia lugha yetu hiyo sawa ndio maana unaongea na unaitumia.

Nchi nyingine wanajivunia lugha zao kwa kuwa wanajitosheleza karibu kwa kila kitu, sisi ni tegemezi hivyo tunahitaji kujua ni nini cha kufanya ili tusiingizwe mjini linapokuja suala la lugha hasa Kiingereza kwa kuwa katika katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kiingereza ni lugha rasmi ya kibiashara.

Kwanini kuwabeza watu wakiongea lugha hiyo? Ujinga au ni nini? tunahitaji ujuzi wa kuwasiliana katika lugha mbali mbali, ukikubali sawa ukikataa ukweli utakutafuna kila utakokwenda. Tunahitaji kutoka hapa tulipo kwa kufahamika kuwa tunajua kuandia Kiigereza kizuri lakini kukiongea ni utata mtupu. Tunahitaji zaidi ya hapo ndugu zanguni.

Awali Mwaisanila

A Personal Career Development specialist, passionate about empowering emerging generations of student, graduates and working class.

Related Articles

Leave a Reply

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents