Habari

Umeme kupanda kwa asilimia 200

Shirika la Umeme nchini (TANESCO), linakusudia kupandisha bei za umeme kwa asilimia 200, endapo litaendelea kupata hasara na kulemewa na madeni.

Na Joseph Mwendapole

 

 

 
Shirika la Umeme nchini (TANESCO), linakusudia kupandisha bei za umeme kwa asilimia 200, endapo litaendelea kupata hasara na kulemewa na madeni.

 

 

 

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dk. Idris Rashid, wakati wa semina ya wabunge kuhusu Muswada wa Sheria za Umeme na Biashara.

 

 

 

Alisema gharama za uzalishaji ni kubwa sana na kwamba bei za umeme wanazotoza kwa sasa haziwezi kufidia gharama za uzalishaji huo.

 

 

 

Alisema shirika hilo limekuwa likipata hasara kila mwaka, hasara ambayo imekuwa ikiongezeka, na kwamba ili kulinusuru linatakiwa kuongeza bei ya umeme kwa wateja wake.

 

 

 

Alitoa mfano kuwa mwaka juzi Shirika lilipata hasara ya Sh. bilioni 183, mwaka jana Sh. bilioni 72, mwaka 2005 Sh. bilioni 0.9, mwaka 2004 Sh. bilioni 15.6, mwaka 2003 Sh. bilioni 177 na mwaka 2002 Sh. bilioni 72.

 

 

 

Alisema mwaka jana waliomba kuongeza bei kwa asilimia 40 wakaruhusiwa kuongeza asilimia 21 tu.

 

 

 

Alisema shirika hilo linatumia asilimia 90 ya mapato yake kununua umeme kutoka makampuni yanayoliuliza umeme shirika hilo.

 

 

 

Makampuni ya wawakezeji ambayo yamekuwa yakiliuzia umeme TANESCO ni pamoja na IPTL, Songas, Richmond na AGGREKO.

 

 

 

Kamati ya Bunge ya Richmond ilionyesha kwamba mikataba ambayo serikali kupitia TANESCO iliingia na makampuni hayo ina upungufu ambao unawanufaisha zaidi wawekezaji na kuwaumiza wananchi wanaolipia bei kubwa ya umeme.

 

 

 

Kamati hiyo iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, ilipendekeza mikataba hiyo ipitiwe upya.

 

 

 

“Hali ikiendelea kuwa mbaya zaidi mwakani tutaomba tuongeze bei kwa asilimia 200 ili angalau wakipunguza waturuhusu tuongeze kwa asilimia 100 kunusuru shirika,“ alisema Dk. Rashid.

 

 

 

Alisema kama serikali haitaki shirika hilo lipandishe bei ya umeme ililipe shirika hilo fedha zinazotumika kuzalisha umeme.

 

 

 

Alisema hatokubali shirika hilo lijiendeshe kwa hasara na kwamba kila ikibidi watalazimika kuongeza bei kwa wateja.

 

 

 

Aidha, Dk. Rashid, alisema kuwa Sh. bilioni 300 ambazo Shirika hilo lilikopeshwa na benki mbalimbali hivi karibuni, zilitumika kulipa madeni ambayo shirika limeyarithi.

 

 

 

Alisema katika miaka mitano ijayo, Shirika hilo linahitaji mtaji wa Sh. trilioni 1.5 ili liweze kumudu kuboresha mfumo wa usafirishaji umeme na usambazaji.

 

 

 

Dk. Rashid alisema ifikapo mwaka 2012 shirika linakusudia liwe na uwezo wa kuwaunganishia umeme wateja 100,000 kila mwaka kulinganisha na sasa ambapo kwa mwaka ni wateja 32,000 wanaounganishiwa.

 

 

 

Alisema asilimia kumi tu ya watanzania ndio wanapata umeme kwa sasa na kwamba miaka mitano ijayo wamepanga kuwaunganishia umeme asilimia 25 ya wateja.

 

 

 

Alisema wanakusudia pia kupunguza kiwango cha umeme kinachopotea kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 23 hadi kufikia asilimia 13 mwaka 2012.

 

 

 

Katika hali iliyowashangaza wabunge waliohudhuria mkutano huo, Dk. Rashid alisema Tanesco inanunua nguzo kutoka Afrika kusini na India kwa kuwa zinauzwa bei rahisi kuliko zinazotoka Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

 

 

 

Alisema wanalazimika kuagiza kutoka nchi hizo kwa kuwa shirika halina uwezo wa kununua nguzo za Tanzania.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents