Habari

Umeme bei juu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imeidhinisha kupanda kwa gharama za umeme kwa asilimia 21.7 kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa asilimia 168 kuanzia Jumanne wiki ijayo.

Faraja Mgwabati

 

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imeidhinisha kupanda kwa gharama za umeme kwa asilimia 21.7 kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa asilimia 168 kuanzia Jumanne wiki ijayo.

 

Kulingana na kiwango hicho kilichopitishwa, hivi sasa wale walio katika kundi la wateja wenye matumizi yasiyozidi uniti 50 kwa mwezi, watakuwa wakinunua kila uniti ya umeme kwa Sh 49 badala ya Sh 40 zinazotumika sasa. Watumiaji wakubwa, watanunua kila uniti kwa Sh 156 badala ya Sh 128.

 

Uamuzi huo umefikiwa jana na Ewura katika kujibu maombi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo Agosti mwaka huu liliomba kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 40 na gharama za kuunganishiwa umeme kwa kati ya asilimia 66 na 281.

 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema mamlaka hiyo imepitia maombi ya Tanesco kwa makini na kuona ni vyema wakapandisha kwa asilimia 21.7 ili kuwe na uwiano wa faida kati ya wananchi na Tanesco.

 

“Tumeona tutoe uamuzi ambao utaisaidia Tanesco kupata fedha kwa ajili ya kujiendesha, lakini bila ya kuwaumiza sana wananchi na wadau wengine watumiaji wa umeme nchini,” alisema Masebu na kuongeza kuwa kiasi walichokadiria kinatosha kwa Tanesco kujiendesha kwa faida.

 

Masebu alisema kutokana na kupanda huko, hivi sasa bei ya umeme wa uniti moja kwa watumiaji wadogo wa majumbani itakuwa Sh 49 badala ya 40 ya sasa . Kwa mtumiaji ambaye atazidisha matumizi yake kwa kila uniti 50 zitakazozidi, atalipa Sh 156 badala ya Sh 128 ya sasa.

 

Alisema kwa matumizi ya kawaida, bei imepanda hadi kufikia Sh 129 kutoka 106 kwa uniti moja, huku gharama ya huduma kwa mwezi itapanda kutoka Sh 1,892 ya sasa hadi Sh 2,303. Mkurugenzi huyo alisema kwa wateja wanaotumia msongo mdogo, watalipa gharama ya huduma ya Sh 8,534 badala ile ya sasa ambayo ni Sh 7,012 na bei kwa kila uniti moja itakuwa ni Sh 85 badala ya 70.

 

Alisema kwa watumiaji wa msongo mkubwa, gharama ya huduma kwa mwezi itakuwa kama ya msongo mdogo, lakini gharama ya uniti moja itakuwa Sh 79 badala ya 65. Kuhusu kupanda kwa bei ya umeme Zanzibar kwa asilimia 168, kutoka Sh 28 hadi Sh 75 kwa kilowati moja, Masebu alisema hiyo inatokana na wateja wa Zanzibar ambao ni Shirika la Umeme na Mafuta la visiwani humo kulipa bei ndogo ikilinganishwa na hali halisi ya gharama za uendeshaji.

 

“Pamoja na Zanzibar kuongezewa gharama kubwa, lakini bado bei hiyo ipo chini ukilinganisha na zinazolipwa na watumiaji wa umeme wa bara,” alisema Masebu. Sambamba na kutangaza bei hizo mpya za umeme, Ewura pia imeiagiza Tanesco kufanya utafiti wa kina kutambua viwango vya upotevu wa umeme ili kupunguza kiasi kikubwa cha umeme kinachopotea sasa na kuwasilisha taarifa ya utafiti huo ndani ya mwaka mmoja.

 

Ewura pia imeiagiza Tanesco kuhakikisha ifikapo Machi mwakani, iwe imewasilisha Ewura uthibitisho kwamba imeanza kufunga makasha ya dira za umeme zenye teknolojia ya usalama zinazozuia wizi wa umeme. Pia imetakiwa kuwa imewasilisha uthibitisho wa mpango wa ukarabati na uboreshaji wa mitambo kutokana na kiwango cha Sh bilioni 56 zitakazopatikana kwa mujibu wa gharama zilizoidhinishwa na Ewura.

 

Kuanzia Januari mosi, 2008, Tanesco pia watatakiwa kuwasilisha Ewura ripoti za robo mwaka zikiwa na mchanganuo wa kila mwezi kuhusu ununuzi, uzalishaji na jinsi inavyohakiki uwiano wa kuchanganya teknolojia za kuzalisha umeme. Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, hakuweza kupatikana kuzungumzia uamuzi huo lakini taarifa kutoka ndani ya ofisi yake, zilisema bado walikuwa hawajapata barua kutoka Ewura. Awali Masebu alisema Tanesco walishapewa taarifa juzi.

 

Uamuzi wa Ewura umefikiwa baada ya kuendesha mchakato wa miezi mitatu kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali katika miji mikuu ya mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tanesco na wananchi wana nafasi ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Ushindani wa Haki, kama kati yao, au wote hawatakubaliana na uamuzi huo wa Ewura.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents