Siasa

Ufisadi BoT: Waziri wa Fedha hana mpango wa kujiuzulu

PAMOJA na shinikizo la wapinzani kutaka ajiuzulu, Waziri wa Fedha Zakia Meghji, amesema hafikirii kuachia nafasi hiyo kutokana na tuhuma za ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Na Ramadhan Semtawa

 

PAMOJA na shinikizo la wapinzani kutaka ajiuzulu, Waziri wa Fedha Zakia Meghji, amesema hafikirii kuachia nafasi hiyo kutokana na tuhuma za ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

 

Badala yake, Meghji alifafanua kwamba hata Rais Jakaya Kikwete, akimwondoa katika nafasi hiyo bado rekodi yake wizarani hapo itakuwa ni ya mtu mwadilifu na si fisadi.

 

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Meghji alisema haoni sababu ya kutakiwa kujiuzulu kwa ajili ya tuhuma hizo kwani ndiye aliyeshiriki kikamilifu kutaka ukaguzi wa kimataifa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT.

 

Meghji alifafanua kuwa shinikizo la kujiuzulu kwa kupewa taarifa potofu na Gavana aliyepita Daud Ballali kwa kuthibitisha malipo ya karibu sh 40 bilioni kwa Kampuni ya Kagoda Agriculture, halina msingi kwa kuwa alitengua barua yake ya awali siku nne baada ya kuthibitisha kulikuwa na uongo katika matumizi fedha hizo.

 

“Sioni sababu ya kujiuzulu na siwezi kujiuzulu, kama ni barua yangu ya kwanza kuthibitisha malipo kwa Kagoda niliitengua siku nne baada ya kubaini ni uongo. Ni sawa na Rais anamteua mtu halafu anatengua baada ya kubaini aliyemteua hafai,” alisema Meghji na kuongeza:

 

“Lakini kama ningekuwa nimeidhinisha mimi malipo hayo ningejiuzulu, mimi niliombwa kuthibitisha malipo ambayo yalishafanyika, lakini nikabaini uongo nikatengua barua yangu,” alisisitiza.

 

Waziri Meghji alifafanua kwamba, kutokana na mfumo wa utendaji kazi serikalini na nafasi aliyokuwanayo Ballali kama Mshauri Mkuu wa Mambo ya Uchumi wa nchi katika BoT na kazi ambayo fedha hizo imeombewa ambayo ni kwa ajili ya Usalama wa nchi, haikuwa rahisi kuweza kukataa lakini alipobaini kuwa ni uongo aitengua barua ya awali.

 

“Hapa naomba watu waelewe, sikuidhinisha malipo ya pesa hizo kwa Kagoda bali kuthibitisha malipo ambayo yalishalipwa mwaka 2005, Ballali kama Mshauri Mkuu wa Mambo ya Uchumi, alikuja akanitaka niandike barua kueleza kwamba fedha hizo zililipwa kwa ajili ya shughuli za usalama wa nchi,” alisema.

 

Alisema malipo ya fedha hizo kwa Kagoda ambazo zililipwa mwaka huo 2005, utata wake ulibainika katika ukaguzi wa ya Kampuni ya Doloitte &Touche na kuongeza kwamba hakuwahi kusimamisha au kutengua zabuni ya kampuni hiyo ya ukaguzi ndani ya BoT.

 

“Sikuwahi kutengua au kusitisha mkataba wa BoT na Deloitte&Touche, hawa ndiyo wamegundua upotevu wa fedha hizi na wametusaidia, ndiyo maana pia serikali ikachukua taarifa ya kampuni hii na kuamua kufanya ukaguzi mzima katika EPA ambao ulifanywa na Ernst&Young,” alisisitiza.

 

Alisema BoT ilikuwa na mkataba wake na Deloitte&Touche, hivyo haikuwa rahisi kwa yeye kuutengua na kuongeza kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) chini ya sheria mpya ndiye mwenye mamlaka ya kuteua kampuni ya ukaguzi.

 

Waziri Meghji alipoulizwa vipi Kampuni ya Kilimo ya Kagoda inaweza kupewa fedha kwa madai ya shughuli za usalama wa nchi, alijibu: “Mambo ya usalama yanaweza kufanywa hata na kampuni au taasisi inayojifanya ina tafiti mambo ya elimu, usalama ni mambo mapana,” alisema.

 

Katika hatua nyingine, serikali imesitisha malipo ya huduma za matibabu kwa Ballali kutokana na sasa kutokuwa Gavana.

 

Waziri Meghji alipoulizwa alijibu: “Nitalifuatilia kwa karibu kwa watu wa BoT wao wanaweza kuwa na taarifa zaidi.”

 

Alipoulizwa tena, Ballali amelazwa katika hospitali gani na anaumwa nini, alisema ni vigumu kueleza kwa sasa.

 

Kauli hiyo ya Meghji ni sawa na ambayo ilitolewa wiki iliyopita Ikulu na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye naye alikataa kueleza maradhi ya Ballali na hospitali aliyolazwa.

 

Ukiacha Meghji na Luhanjo, ugonjwa wa Ballali na hospitali aliyolazwa umezidi kuwa siri kutokana na pia na Gavana mpya wa BoT Profesa Benno Ndulu, kukataa kueleza maradhi na hospitali.

 

Sakata la ufisadi katika BoT hasa wa zaidi ya sh 133 bilioni, umeibua mjadala mzito nchini kufuatia uamuzi wa Rais Jakaya Kiwete kumwachisha kazi Ballali, baadhi ya wanasiasa wa kambi ya upinzani wametaka hatua zaidi kwa wahusika wengine huku wakimtaja Meghji na Basil Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati wa ufisadi huo, nao wajiuzulu.

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents