Bongo Movie

Jumba la Filamu: Uchambuzi wa filamu ‘Bado Natafuta’ ya Salim Ahmed ‘Gabo’

Katika Jumba la Filamu leo, tunaangazia filamu ya ‘Bado Natafuta’ iliyotayarishwa na kampuni ya Jerusalem. Ni filamu nzuri inayoelezea mkasa wa mapenzi kati ya watu wawili wenye maisha tofauti,binti akitoka katika maisha ya kitajiri na bwana akitoka katika maisha ya kimasikini.

bado_natafuta

Bado Natafuta ni filamu iliyoongozwa na muigizaji mkongwe wa filamu, Jacob Stephen aka JB na mtunzi wa hadithi hii ni Danil Manage. Ni hadithi inayoelezea maisha ya halisi ya mapenzi jinsi yalivyo na nguvu.

Salim Ahmed aka ‘Gabo’ ambaye ndani ya filamu hii ametumia jina la James ndiye mhusika mkuu.Amevaa uhusika wa kijana masikini muuza maji aliyetumia matatizo yake kama changamoto nakuja kufanikawa.Hii ilikuwa baada ya Patricia ‘Shamsa Ford’ mtoto wa familia ya kitajiri ambaye alikuwa daktari kumpenda James aliyempa ujauzito ilhali James hana mbele wala nyuma.

Washiriki wengine ni Patcho Mwamba, Zuberu Mohammed, Wellu Sengo, Faridaq Sabu, Careena Hussein, Magdalena Roy, Mariam Adam na Hansley Andrew.

Hadithi

Hadithi ni nzuri. Mtunzi wa hadithi aliangalia maisha ya halisi ya mapenzi katika jamii yanayokabiliwa na migogoro, shida chuki na furaha; vyote vilionekana katika hadithi hii. Tumemuona Patricia alivyozimika na penzi la muuza maji James,kitu ambacho kwa hali ya maisha ya kawaida hapa Tanzania na duniani kote hutokea kwa nadra.

James kacheza kama kijana muuza maji na fundi magari mwenye maisha duni.Biashara ya maji na ufundi magari wake ulimuunganisha kimapenzi na mwanadada ‘Patricia’ ambaye ni daktari. Anajikuta akibeba ujauzito wa James,hali ambayo inamfanya James kumuaga mwanadada huyo na kwenda kutafuta maisha ili atakapojifungua, mtoto aje kupata maisha bora kutoka kwa wazazi wake.

Shamsa Ford ni mmoja ya wasanii wa filamu hapa nchini anayefanya vizuri. Katika filamu hii ametumia jina la Patricia. Baada ya Patricia kupewa ujauzito na James, watu wengi wanashangazwa akiwemo mdogo wake na rafiki zake, wakijiuliza ni kwa nini amempenda James muuza maji,wakati alikuwa nafasi wa kumpata mwanaume mwenye pesa.

Baada ya kujifungua na kukaa muda mrefu bila mawasilano na James, Patricia anapata mchumba mwingine, hali ambayo inamfanya James kushindwa kurudi nyumbani moja kwa moja akitokea katika safari ya muda mrefu ya kwenda kutafuta pesa ili waje kuishi pamoja na mtoto wao.

James anaendelea kukaa katika hoteli akitafuta jinsi ya kuoanana na Patricia,wakati huo huo anaona bora amtafute mtoto wake ili ajue Patricia naishi na nani. Kwakuwa kabla ya kuondoka James aliacha jina la mwanaye pindi atakapozaliwa, ilimpa urahisi kumfuatilia mtoto wake katika shule mbalimbali na baadaye kufanikiwa kupata.

James anaendelea kuwa karibu na mtoto wake, mpaka pale mtoto anapokuja kumjulisha kuwa mama yake anaishi na ‘Uncle’ ambaye ni mchumba mpya wa Patricia na kumfanya James ajisikie vibaya sana. Wakati ametulia chumbani kwenye hoteli aliyofikia ghafla aliingiliwa na mwanadada aliyekyuwa akijipendekeza kwa James. hali ambayo inaleta tafrani.

“Kwani wewe unajiuza?” anauliza James na huku dada huyo akijibu unanitukana? “Siyo kama nakutukana, swali nilokuuliza ni swali la msingi sana, maana toka umefika nakuona mara baby mara sweety mara honey, ndio unajibebisha tu, ndio maana nikakuuliza swali la msingi kwani wewe unajiuza?” anasema James.

Wakati James anaendelea kumuuliza maswali msichana huyo, Patricia anawasili katika hoteli hiyo baada ya kupewa taarifa na rafiki yake kwamba James yupo hapo hotelini. Kwakuwa mlango haukufungwa Patricia anausukuma mlango na kuingia ndani,ndipo wanapopishana na yule dada hapo mlangoni. James anabaki ameduwaa na Patricia akiwa na mshtuko pia. Kinachoendelea ni ugomvi kati ya Patricia na James.

James anajaribu kumbembeleza Patricia, “Moyo wangu ulikuwa mbali lakini unaendelea kutambua, uwepo wa thamani ya mapenzi yangu kwako, moyo huu huu uliweza kugusa wa kwako wakati hauna kitu, na moyo huu huu ndio umerudi tena kwa mara nyingine kukumbusha mateso uliyopata wakati uko mbali na mimi. Moyo wangu umekubali kusamahe, kwanini wa kwako usisamehe?” James Anajaribu kumbeleza Patricia.

Patricia kwa hasira anarudi nyumbani nakumwambia mpenzi wake anayeishi naye ili wavalishane pete ili ajaribu kumsahau James. Nae James akiwa mwenye hasira anamtembelea rafiki yake ili apate ushauri. “Unajua watu wengine wanatafuta mke wa kuishi naye, lakini mimi natafuta mwanamke ambaye siwezi kuishi bila huyo mwanamke,” anasema.

Rafiki anamshauri James waelekee hukohuko ambako Patricia anavishwa pete ili akaseme ya moyoni mbele ya kadamnasi.

Baada ya James kumuona Patricia, anaamua kuongea mbele ya umati mkubwa wa watu: Mapenzi yanauma asikwambie mtu kila mtu anaelewa ,watu wote wamekuja kukuangalieni ninyi hapo sababu ya mapenzi tu na mimi kuja kote huku ni kwaajili ya mapenzi nakupenda sana mke wangu.” Maneno hayo yanamfanya James akabidhiwe jiko lake na mtoto wake.

USAILI

Mtu wa usaili (Casting Director) alifanikiwa kuchagua watu waliozitendea haki nafasi zao. Pongezi kwake kwasababu kila mshiriki alionyesha sababu ya kuwepo katika nafasi aliyopewa.

MAVAZI

Mtu wa mavazi (Costumes Director) alifanikiwa kuwavalisha wasanii, anastahili pongezi, wasanii walipendeza na kuonekana.Kila mhusika alivalishwa nguo kutokana na nafasi aliyoicheza. Hiki ni kipengele kimoja kimeifanya filamu iwevutie kutokana na wahusika kuwa ‘Natural’


MAPAMBO (Makeup)

Mtu wa mapambo alifanya kile kinachostahili, aliweza kuwatengeneza vizuri wasanii na kuonekana vizuri hasa sehemu ambayo kichaa alicheza.


MANDHARI

Mtu wa mandhari (Location manager) alifanikiwa sana katika kutafuta sehemu za kurekodi, zilistahili kulingana na matukio yaliyoonyeshwa katika filamu hiyo, anastahili pongezi.

MWANGA

Mtu wa mwanga alifanikiwa katika kupanga taa na kufanikiwa kuweka mwanga sahihi na kuwamulika vyema katika matukio husika, anastahili pongezi zake.

SAUTI

Mtu wa sauti (Soundman) alikuwa poa, sauti katika filamu hii imesikika vizuri na kumfanya mtazamaji asiwe na usumbufu wa kupandisha sauti na kushusha mara kwa mara.

MHARIRI

Mhariri alifanya kazi yake vema, ndio maana hatuoni makosa yakijitokeza na kuwa mengi kwa kiwango cha juu.

MUONGOZAJI

Muongozaji (Director) ni mtu muhimu sana katika kuhakikisha filamu inakuwa bora kulingana na hadithi husika kwa kulinda wazo la mwandishi au mtunzi, ukiangalia filamu hii imefanya vizuri sana sifa zinaenda kwa muongozaji,wahusika walikuwa ‘natural’ sana.

Moani

Bado Natafuta ni filamu nzuri sana. Nadiriki kusema ni miongoni mwa filamu bora za mwaka 2013.Nakumbuka wakati Bongo5 inaandaa filamu zilizofanya vizuri 2013, wauzaji na wasambazaji wa filamu walisema Bado Natafuta ni filamu inayopendwa mno kutokana na wahusika kubeba uhalisia hali iliyoitanya filamu hii kupata umaarufu mkubwa.

Salim Ahmed aka Gabo ni miongoni mwa waigazaji wanaofanya vizuri. Kupitia filamu ya Bado Natafuta alichaguliwa kushiriki katika Action and Cut viewer’s Choice Award ‘ACV AWARD’ 2013, katika kipengele cha muigizaji bora.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents