Burudani

Uchambuzi: ‘Kwenu Vipi’ ya Stamina na Nay wa Mitego ni ‘Part 2’ ya ‘Muziki Gani’

Muziki Gani ya Nay wa Mitego na Diamond Platnumz iliwakilisha majibizano kati ya wasanii wanaofanya hip hop na wale wanaofanya Bongo Flava. Lakini kwakuwa majibizano kama hayo yanaendelea kila siku baina ya wale wanaofanya hip hop ambayo sasa imegawanyika pia, Stamina na Nay wameamua kuyaweka kwenye wimbo mpya ‘Kwenu Vipi’.

10499233_1456909937896319_1974954013_n

Katika ngoma hii Stamina anawakilisha kundi la wasanii wa hip hop waliobaki na misimamo ya kufanya hip hop ngumu ambayo hutafsiriwa kama muziki usiokuwa rafiki na biashara wakati Nay wa Mitego akiwakilisha wana hip hop waliobadilika kidogo kwendana na soko na kulainisha muziki wao kwa kutumia beat zenye ladha ya Bongo Flava ama na wao kuimba kabisa.

Mara nyingi kundi linalowakilishwa na Nay wa Mitego limekuwa likitafsiriwa kama lenye mafanikio ukilinganisha na wale wanaoendelea kukaza kwa midundo migumu na mashairi ya kiufundi zaidi.

Katika mistari ya Stamina, anasikika akizitolea mfano ‘Nakula Ujana’ ya Nay na ‘Pombe Yangu’ ya Madee kuwa miongoni mwa nyimbo zisizoelimisha jamii na anadai kuwa zinabebwa. Naye Nay wa Mitego akiutaja wimbo wa Professor J ‘Kamiligado’ kuwa ulifanikiwa pamoja na kwamba mchawi huyo wa rhymes aliimba.

Katika mistari mingine Nay anasema rappers wenye misimamo ya hip hop ngumu wameendelea kuishi kwa wazazi wao kwakuwa muziki hauwalipi na huku Stamina akimpa dongo Nay kuwa alikimbia hip hop halisi baada ya kugundua anafichwa.

“Kwanza hamtambui kwamba huu muziki ni kazi, na ndio maana mnakatazwa na wazazi, unafanya muziki mwaka wa kumi huna hata Bajaj, nyie sio wasanii ni wasindikizaji,”
anarap Nay wa Mitego. “Kwa kupost picha Insta (gram) hilo mnaongoza, utasikia mjengo wangu mpya kumbe umepanga unajiongeza,” anachana Stamina.

Nay anamjibu: Eti mnajifanya mnakaza huku mnakufa njaa, hakuna mnachopata zaidi ya sifa kwenye mitaa, kwanza mnatudhalilisha kutwa mnapiga mizinga Umarekani mwingi mpaka mnakula unga.”

“Si bora sisi unga kuliko nyie mapunga, hamna style, hamna swag wala hamjui kutunga, kwa kuongeza sifuri kwa hilo mnaujasiri hata video ya milioni 2 utaskia milioni 200,” anajibu Stamina.

Mwisho Godzilla anamalizia kwa outro na kusisitiza umoja kati ya wasanii wote bila kuzingatia muziki wanaofanya.

Usikilize wimbo huo hapa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents