Habari

Twaweza yatoa utafiti kuhusu wananchi na haki ya kupata habari

Tafiti mpya ya Twaweza ya mwaka 2016 imebaini mambo mengi kuhusu wananchi na haki ya kupata habari.
career-in-mass-media

Hii ndio taarifa ya Twaweza

Ingawa sheria inaipa mamlaka serikali kulifungia gazeti bila kuhojiwa, asilimia 91 ya wananchi wanasema kabla ya gazeti kufungiwa suala hilo lijadiliwe kwanza mahakamani.

Takribani wananchi 8 kati ya 10 (78%) wanaamini upatikanaji wa habari utapunguza vitendo viovu pamoja na rushwa, huku wananchi 6 kati ya 10 (60%) wakisema serikali iwe na mamlaka tu ya kuzuia habari ambazo ni muhimu kwa usalama wa taifa. Hivyo basi kwa kiasi kikubwa wananchi wanaunga mkono suala la uwazi na uwajibikaji.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia utafiti wake unaopatikana kwenye muhtasari wenye kichwa cha habari Mwangaza, Wananchi na Haki ya kupata habari. Muhtasari huo unatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,811 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 10 na tarehe 25 Februari 2016.

Aidha, zaidi ya nusu ya wananchi wanaamini kwamba kuna uwezekano wa kupatikana kwa taarifa muhimu kama zifuatazo: Namna ya kusajili uzazi (71%), namna ya kutoa taarifa juu ya kituo cha maji kilichoharibika (63%), na namna ya kutoa taarifa juu ya vitendo vya rushwa (56%). Hata hivyo chini ya nusu ya wananchi wanaamini wanaweza kupata taarifa kuhusu bajeti za wilaya, mipango na matumizi (42%), kiwango cha ruzuku kilichopelekwa kwenye shule zao (39%) au upungufu wa dawa kwenye vituo vya afya (35%).

Cha kushangaza ni kwamba imani hiyo haitokani na uzoefu wao kwani zaidi ya wananchi 8 kati ya 10 waliohojiwa hawajawahi kufika kwenye ofisi ya mamlaka za maji, shule za msingi za umma, vituo vya afya, wala ofisi za serikali za mitaa kutafuta taarifa zozote. Wananchi wengi wameonekana kutegemea zaidi redio (70%) na kwa kiwango kidogo runinga (21%) kama vyanzo vyao vikuu vya kupata habari.

Redio inaaminika na asilimia 80 ya wananchi na runinga inaaminika na asilimia 73 ya wananchi, tofauti na magazeti yanaaminika kwa asilimia 27 tu ya wananchi. Japokuwa mitandao ya kijamii inaaminika kwa kiasi kidogo sana na kutumiwa kwa kiwango cha chini kama chanzo cha habari, utafiti wa Sauti za Wananchi umebaini kuwa asilimia 47 ya wananchi hutumia mitandao ya kijamii huku asilimia 53 wakiwa hawatumii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents