Burudani

Tunamuongelea Hanscana kwa kiwango kile kile tulichokuwa tukimuongelea Nisher mwaka jana

Unakumbuka mwaka jana jinsi jina la Nisher lililivyokuwa likivuma? Muongozaji huyo wa video kutoka Arusha alikuwa gumzo kwenye midomo ya mashabiki wengi wa muziki hapa nchini kutokana na uwezo wake tofauti katika kutengeneza video zake.

10952939_939325492764846_211416287_n
Nisher

Mwaka 2014 ulikuwa ni mwaka wake, na ndio maana alifanikiwa kushinda tuzo ya muongozaji wa video za muziki zinazopendwa kwenye Tuzo za Watu.

Pamoja na zingine, video yake bora ya mwaka jana ilikuwa ni ya wimbo wa Weusi, Nje ya Box. Utengezaji wake tofauti wa video ulimfanya ajikusanyie mashabiki kibao lakini pia akawa tishio kwa waongozaji waliokuwepo kitambo.

Tunakumbuka pia jinsi ambavyo Nisher na Adam Juma waliingia kwenye vita vya maneno kwenye mitandao ya kijamii. Ni ukweli kuwa pamoja na Adam Juma kuwa na heshima yake isiyokanwa, Nisher aligeuka kuwa tishio lake kubwa.

Nisher aliwapa changamoto kubwa waongozaji wengine wengi na kuwapa somo kuwa ili kutengeneza video itakayokuwa gumzo kwa wengi, ni lazima muongozaji awe ‘aggressive’ na awe na mchango wake pia katika kuipromote video anayoitengeneza bila kumwachia kazi hiyo msanii peke yake.

Mwaka 2015, mambo yamebadilika na ule usemi wa Kiingereza usemao ‘what goes around comes around’ umejidhihirisha. Nisher anakumbana na ushindani mkubwa kwa sasa kutoka kwa muongozaji aliyetokea kukubalika na wasanii wengi, Hanscana.

10979611_403674746460561_1913112252_n
Hanscana

Siwezi kumsahau pia rafiki yake Khalfan ambao kwa pamoja wameunda timu machachari ya waongozaji wa video Tanzania. Tofauti na Khalfan ambaye ni mkimya, pengine ndio maana Hanscana anaongelewa zaidi kwakuwa ana character na attitude kama ya Nisher. Wote wanajiamini na wanapenda drama!

10990645_352717144916096_1281256723_n

Japo Nisher aliwahi kutuambia kuwa Hanscana si tishio kwake, kwa wengi inaonekana wazi kuwa kazi nyingi ambazo mwaka huu zingetua mikononi mwa Nisher, zimeenda kwa Hanscana. Na tayari Nisher amekiri kuwa hiki ni kipindi kigumu zaidi kibiashara.

“Napenda kuwashukuru sana kwa comments zenu, zimenipa nguvu ya kuendelea na vita, hasa wakati huu ambapo biashara hii imeshaingia ukungu,” Nisher ambaye video ya Bongo Hip Hop ya Fid Q aliyoingoza imepokelewa kwa mchanganyiko wa maoni hasi na chanya, ameandika kwenye Instagram.

“Napenda pia kumshukuru sana uncle wangu @fidq,” ameongeza. “Since day one nakutana naye nilianza kumwita uncle, sijui kwanini but kuna namna tumekua na connection nzuri sana mimi na yeye. Ni mtu mmoja msikivu sana na anapenda watu wenye akili nyingi. Pia ni mcheshi sana. So thank you uncle kwa kunipa chance ya kuonyesha uwezo wangu katika kipindi hiki kigumu kibiashara, na kukubali kuingia gharama zote ili kufanikisha zoezi hili pia kwa kuniamini kupita nilivyotegemea. Ungeweza kufanya kazi hii na mwingine yeyote but ulinichagua mimi.”

Kwanini Nisher anaamini kuwa biashara yao imeingia ukungu na imekuwa ngumu? Pengine jibu la uhakika linapatikana baada ya kulitaja jina ‘Hanscana’ muongozaji ambaye Nisher anamuita ‘Printer’.

11049202_809515912476666_1134680822_n
Hanscana akiwa location na Roma

Nisher na Hanscana haziivi. Wawili hawa wamekuwa wakitupiana vijembe vya hapa na pale kwenye mitandao ya kijamii. Lakini inavyoonekana, huu ni mchezo wa timing, ukilemaa unaachwa feli! Ukweli huo unawafanya wawili hawa kulala usingizi huku jicho moja likiwa wazi kama nyangumi ili kuepuka kupitwa kwenye marathon.

Ni hivi karibuni tu baada ya kuongoza video ya wimbo wa Vanessa Mdee na Barnaba ya wimbo wao ‘Siri’, Hanscana amepata deal la kuongoza video ya Diamond Platnumz – staa ambaye ukimtoa Adam Juma na Raqey, hakuna muongozaji mwingine wa Tanzania aliyewahi kuongoza video zake.
Kwa ukubwa ambao Diamond amefikia na kuamua kumchukua Hanscana kuongoza video yake, ni wazi kuwa kijana huyo ambaye kama Nisher, naye anatokea jijini Arusha, amekwiva.

Kitendo cha muongozaji huyo mpya wa video za muziki kupewa jukumu la kuongoza video ya Diamond, ni zawadi kubwa zaidi anayoweza kuipata katika career yake kuzidi hata fedha atakayolipwa. Kama ilivyokuwa kwa Sheddy Clever, Hanscana atapata nafasi ya kujulikana Afrika nzima kupitia video hiyo.

Lakini bado Nisher ana nafasi nyingine ya kutisha mwaka huu kupitia msanii aliyeanza kujulikana barani Afrika kabla ya Diamond. Nisher ataongoza video ya wimbo mpya wa AY, Zigo.

11007952_871307346269830_1253932777_n

Lakini kitu ambacho watu wanapaswa kujua ni kuwa ukiangalia video za Hanscana na nduguye Khalfan, utagundua kuwa vijana hawa walikuwa inspired na namna Nisher anavyochukua na kuhariri picha zake. Kama anavyofanya Nisher, Hanscana naye ni mzuri katika kuchagua shots za kueleweka. Na siku zote mshindani wako mkubwa ni yule anayekufahamu vyema.

Kitu pekee ambacho Hanscana ana advantage dhidi ya Nisher ni kuwa yeye anaishi Dar es Salam, tofauti na mwenzie ambaye bado anaishi Arusha na hivyo huja Dar kwa kipindi maalum tu. Kibiashara, Hanscana ana advantage kwakuwa upatikanaji wake ni wa uhakika. Kwa Nisher inakuwa ngumu kiasi kwa wasanii wanaomuhitaji akiwa Arusha kwakuwa huwabidi waingie gharama zingine zikiwemo nauli ya ndege ya kuja na kurudi pamoja na gharama za hoteli huku gharama za kutengeneza video zikiwa peke yake.

Wasanii wenye bajeti ndogo hili limekuwa likiwazuia kufanya kazi na muongozaji huyo. Nadhani kwa Nisher, ukungu anaouona kwenye biashara hii unaweza kufutika iwapo atalipa uzito suala la kuhamishia makazi Dar.

Kwahiyo kama alivyosema Nisher kwenye maelezo yake, kilichopo sasa ni vita. Kitu kizuri katika mazingira kama haya ni kuwa ushindani katika biashara yoyote huleta faida kwa mteja. Maana yake ni kuwa tutegemee video kali mwaka huu kutoka kwa Nisher na Hanscana. Kadri ushindani unavyokuwa mkubwa, ndivyo ubora wa video za muziki unavyozidi kuimarika.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents