Siasa

TRA kuchunguza waliochota BoT

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeagizwa kufanya uchunguzi wa kina kubaini mienendo ya ulipaji kodi wa kampuni 22 zilizohusika katika ubadhirifu wa Sh bilioni 133 za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia akaunti yake ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Maulid Ahmed, Dodoma

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeagizwa kufanya uchunguzi wa kina kubaini mienendo ya ulipaji kodi wa kampuni 22 zilizohusika katika ubadhirifu wa Sh bilioni 133 za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia akaunti yake ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

 

Sambamba na hilo, pia Wizara ya Fedha imeielekeza BoT kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa serikalini kuhusu hatua zilizochukuliwa kwa benki za biashara zilizohusika kupokea fedha kutoka makampuni husika, endapo sheria, taratibu na kanuni kuhusu udhibiti wa fedha haramu, vilizingatiwa.

 

Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, aliwaeleza hayo wabunge jana wakati akitoa kauli yake juu ya sakata la ubadhirifu wa fedha za BoT, akisema agizo hilo limetolewa na wizara yake kwa TRA na kuongeza kuwa, “endapo itabainika kuwapo ukwepaji wa kodi, hatua za kisheria zitachukuliwa.”

 

Kwa mujibu wa taarifa ya wakaguzi wa Ernst and Young ambao iliiwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowapa kazi hiyo ambao nao waliiwasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete aliyechukua hatua ya kumfukuza kazi Gavana Mkuu wa BoT, Daudi Ballali, kampuni 22 za nchini katika mwaka 2005 zililipwa Sh 133,015,186,220.74 isivyo halali.

 

Kampuni hizo ni Bencon International Limited of Tanzania, V.B & Associates Company Limited of Tanzania, Bina Resorts Limited of Tanzania, Venus Hotel Limited of Tanzania, Njake Hotel & Tours Limited, Maltan Mining Company Limited of Tanzania, Money Planners and Consultants, Bora Hotels and Apartments Limited.

 

Nyingine ni B.V Holdings Limited, Ndovu Soaps Limited, Navy Cut Tobacco(T) Limited of Tanzania, Changanyikeni Residential Complex Limited, Kagoda Agriculture Limited, G & T International Limited, Excellent Services Limited, Mibale Farm, Liquidity Service Limited, Clayton Marketing Limited, M/S Rashtas(T) Limited, Malegesi Law Chambers Advocates, Kiloloma & Brother na Karnel Limited.

 

Katika ukaguzi, ilibainika kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh 90,359,078,804 zililipwa kwa kampuni 13 ambazo zilitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kughushi. Pia ukaguzi huo ulibaini kuwa kampuni tisa zilizolipwa Sh 42,656,107,417 hazikuwa na nyaraka ya kuonyesha stahili ya malipo na hivyo kuwafanya wakaguzi washindwe kuhakiki uhalali wa malipo hayo.

 

Kutokana na ubadhirifu huo na kufukuzwa kazi kwa Dk. Ballali, Rais alimteua Profesa Benno Ndulu kuwa Gavana na kuagiza Bodi ya benki hiyo ikutane mara moja na kuwachukulia hatua maofisa waliohusika na ubadhirifu huo. Tayari bodi ilishakutana kwa mara ya kwanza Januari 21, mwaka huu.

 

Rais pia aliteua kamati maalumu inayojumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkuu wa Jeshi la Polisi, kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kwa kampuni na watu waliohusika na uhalifu huo. Kamati hiyo ilipewa miezi sita kukamilisha kazi hiyo. Nayo tayari imeshaanza kupokea taarifa kutoka kwa wananchi.

 

Katika taarifa yake ya kurasa tisa aliyoitoa jana bungeni mjini hapa, Waziri Meghji alisema serikali itahakikisha kila mtu au taasisi iliyohusika na ubadhirifu huo anachukuliwa hatua za kisheria na kuwaomba wananchi watoe ushirikiano ili kamati ikamilishe kazi yake na wawe na subira.

 

Baada ya kuwasilisha ripoti hiyo, wabunge walitaka ripoti kamili ya CAG iwasilishwe bungeni ili waijadili kama inavyofanya kwa ripoti nyingine. Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema taarifa hiyo ya Waziri Meghji ni muhtasari, hivyo wabunge wanahitaji taarifa kamili ya CAG waijadili na kutoa mapendekezo yao.

 

Naye Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alisema “Spika naomba mwongozo ingawa sina kanuni hapa, kwa sababu hamjatupatia bado, kauli ya Waziri nzuri, lakini tunataka taarifa kamili ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali iletwe hapa bungeni tuijadili kama tunavyojadili nyingine.”

 

Hata hivyo, Spika Samuel Sitta alikubaliana na wabunge hao na kusema, “yote hayo yalikuwa katika mchakato wa mazungumzo kati yangu na serikali na ndani ya wiki hii tutapata majibu kutoka serikalini, kama serikali inasikia basi imeshasikia.”

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents