Tatiana atua Dar

TatianaMshiriki wa shindano la Big Brother Africa 2, Tatiana Durao, kutoka Angola, amewasili nchini leo, kwa ajili ya maonyesho mawili ya mavazi yatakayofanyika Aprili 25, jijini Arusha na kesho yake jijini Dar es Salaam

Tatiana
 
Mshiriki wa shindano la Big Brother Africa 2, Tatiana Durao, kutoka Angola, amewasili nchini leo, kwa ajili ya maonyesho mawili ya mavazi yatakayofanyika Aprili 25, jijini Arusha na kesho yake jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mratibu wa ujio wa mwanamitindo huyo wa kimataifa, Petter Mwendapole, ziara hiyo ya Tatiana, mbali ya shughuli ya uanamitindo, pia ni uthibitisho wa upendo wa Tatiana kwa Tanzania.

TatianaAidha, aliongeza kuwa, ujio wake Tanzania umechangiwa na kufanya vema kwa mshiriki namba moja wa shindano hilo kutoka Tanzania, Richard aliyekuwa mshindi wa kwanza na kuzoa zaidi ya sh milioni 100.

Akiwa katika jumba la Big Brother Africa 2, nchini Afrika Kusini, Tatiana alikuwa akivaa mavazi yenye bendera ya Tanzania, kuashiria upendo wake kwa Tanzania.

Mwendapole alisema, onyesho la jijini Arusha la Aprili 25, litafanyika kwenye ukumbi wa Naura Spring ambao ni pacha na Hoteli ya kitalii ya Ngurdoto, kabla ya onyesho la pili Aprili 26, litakalofanyika Hoteli ya Movenpick, jijini Dar es Salaam.

Mwendapole alisema, mbali ya kufanya maonyesho hayo, Tatiana pia atatembelea sehemu kadhaa za kitalii kama mbuga ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar.

Tatiana ambaye amekuwa akifanya ziara mbalimbali katika nchi za Afrika, anakuja Tanzania kwa lengo la kujenga urafiki na Watanzania, kama alivyofanya wakati wa shindano la Big Brother Africa 2.

Mbali ya Tanzania, nchi nyingine alizotembelea ni Botswana, Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, Ureno na Visiwa vya Sao Tome.

Aidha, itakumbukwa kuwa, alitembelea nchi ya Zambia na hata kula chakula cha usiku na Rais wa nchi hiyo, Levy Mwanawasa.

Tatiana, pia aliwahi kupongezwa na Rais wa Angola, Jos’e Eduardo Dos Santos na kukaa pamoja.

Wadhamini wa ziara hiyo ya Tatiana ni New Habari Limited, Ubalozi wa Angola, Air Tanzania, Tanzania Breweries Limited (TBL) kupitia kinywaji cha Redds Premium Cold na Impala Hotel.

 

 

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents