Habari

Tanesco kuomba leseni upya

SERIKALI imesema kuwa, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), litalazimika kuomba upya leseni za kuendesha shughuli zake, iwapo sheria mpya ya umeme itapitishwa na Bunge na kusainiwa na rais.

na Ratifa Baranyikwa

 

 

 

SERIKALI imesema kuwa, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), litalazimika kuomba upya leseni za kuendesha shughuli zake, iwapo sheria mpya ya umeme itapitishwa na Bunge na kusainiwa na rais.

 

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

 

Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo mpya, ambayo muswada wake ulikuwa unajadiliwa jana, inatarajia kufungua milango kwa mashirika na kampuni nyingine binafsi kutoa huduma ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme hapa nchini na nje ya nchi, kitu ambacho kitaondoa ukiritimba wa Tanesco kama shirika pekee lililokuwa na haki ya kufanya hivyo.

 

Hata hivyo, akizungumza katika kikao hicho kilicholenga kukusanya maoni ya wadau kuhusu sheria hiyo mpya, Karamagi alisema kuwa, kupitishwa kwa sheria hiyo hakutamaanisha kuwa Tanesco itakuwa imepoteza haki zake kama shirika linalojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa umeme.

 

Akifafanua, alisema kuwa kwa kuwa wadau wengine watatakiwa kuomba leseni ili kupata haki ya kufanya shughuli hizo, Tanesco nayo, kama mdau mpya, itatakiwa kuomba leseni hizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini (EWURA).

 

“Na hii haina maana kwamba Tanesco itanyang’anywa, hapana, ila sheria ikishapita itabidi aombe leseni kwa kila kitu kimoja, kuanzia kusafirisha, ugawaji na usambazaji, tofauti na sasa ambapo ina ‘operate’ kwa ujumla katika vitu vyote,” alisema Karamagi.

 

Awali, akielezea madhumuni ya kutunga sheria hiyo mpya, Karamagi alisema kuwa Sheria ya Umeme iliyokuwa ikitumika, ilitungwa mwaka 1931 na imeshafanyiwa marekebisho mara 11 na kwamba hivi sasa sheria hiyo haikidhi matarajio tena kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza.

 

“Sheria hiyo pia haiendani na sheria ya sasa ya EWURA, pia haiweki wazi mamlaka na shughuli za serikali, mabadiliko ya sasa ni makubwa hatuwezi kuweka viraka tena kwenye sheria ya zamani,” alisema.

 

Karamagi alisema kuwa mkakati wa kuwa na sheria mpya ya umeme unajenga mkakati wa upatikanaji wa umeme bora na wa uhakika na wa bei nafuu kwa kuruhusu makampuni binafsi kutoa huduma ya umeme.

 

Alisema sheria hiyo pia ina mkakati ambao madhumuni yake ni kuondoa ukiritimba ambao upo Tanesco, ambayo peke yake ilikuwa imeruhusiwa kuzalisha kusambaza na kusafirisha umeme.

 

“Sasa kuruhusu sekta binafsi kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme, inaruhusu kuhamasisha biashara ya umeme nchini na nchi nyingine,” alisema.

 

Aidha, baadhi ya wadau waliotoa maoni juu ya sheria hiyo, waliipongeza serikali kwa hatua iliyochukua, huku baadhi yao wakisema kuwa sheria hiyo imechelewa kwa kile walichokieleza kuwa ucheleweshaji wa huduma na gharama kubwa zinazotozwa na Tanesco hivi sasa.

 

“Ilifika kipindi tulikuwa tunabembeleza Tanesco haki yetu, mazingira ambayo yalitengeneza rushwa,” alisema mmoja wa wadau.

 

Hata hivyo, walionyesha wasiwasi juu ya udhibiti wa gharama endapo kampuni binafsi zitaruhusiwa, kitu ambacho Karamagi alisema sheria ya EWURA inaipa nguvu mamlaka hiyo kudhibiti bei na kwamba sheria hiyo hairuhusu mwekezaji kupanga bei.

 

Mbali na hayo, pia alisema kuwa sheria hiyo itawabana wawekezaji ambao watasitisha kutoa huduma bila sababu maalum, pia inalinda haki za mtumiaji.

 

Watu wachache walijitokeza kutoa maoni juu ya muswada huo, hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, William Shelukindo (Bumbuli-CCM), alisema kuwa endapo kuna mtu yeyote anayetaka kuwaandikia maoni, basi afanye hivyo na kamati itashughulikia.

 

Mkutano huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo, Mkurugenzi wa Tanesco, Dk. Idris Rashid, Mkurugenzi wa EWURA, Nasibu Masebu, watu mbalimbali kutoka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), wanasheria kutoka Wizara ya Madini na wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents