Habari

Taasisi ya Mama Salma Kikwete yakanusha kukwepa kodi

Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti moja linalochapishwa kila wiki kwa lugha ya Kiswahili kuwa Mwenyekiti wake, Salma Kikwete ana mzigo mkubwa bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi.
img_9379
Mwenyekiti wa WAMA, Salma Kikwete

Taarifa ya Wama iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mtendaji wake Daudi Nassib, ilisema taarifa hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo gazeti hilo lilichapisha habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari “Mali za Salma Kikwete kuuzwa kwa mnada?” katika toleo lake namba 486 la Novemba 30, mwaka huu “Kumetolewa madai eti kwamba taasisi ya Wama inayoongozwa na Salma Kikwete inao mzigo mkubwa bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi.

Na kwa sababu hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania imepanga kuuza mali hizo. “Kwa niaba ya Taasisi ya Wama napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote. “Kwa maoni yetu gazeti hilo lina dhamira mbaya dhidi ya Taasisi ya Wama na Mwenyekiti wake Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na kuchafua majina na sifa ya taasisi yetu na kiongozi wake.”

Katibu mtendaji huyo alisema ukweli kuhusu jambo hilo ni kwamba, Wama ilitumiwa maboksi 11 ya vitabu vikiwa ni zawadi kutoka Taasisi ya Nakayama ya Japan ambayo ndiyo iliyofadhili ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wama-Nakayama iliyopo Nyamisati, Kibiti na yalishatolewa bandarini yangu Agosti 10 mwaka na tayari vitabu viko shuleni na vinatumika.

“Hakuna mzigo wowote wa Taasisi ya Wama uliopo bandarini unaosubiri kutolewa wala kuuzwa na TRA,” imesema sehemu ya taarifa hiyo na kulitaka gazeti hilo kuomba radhi kwa Salma Kikwete na kwa Wama kutokana na taarifa hizo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents