Burudani

Survival of the fittest: Ushindani wa redio za Dar kuongezeka maradufu 2015

Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania haungozi kwa joto, foleni, mzunguko mkubwa wa fedha na mishemishe pekee, bali pia vituo vingi vya redio na TV.

radio-station-microphone

Miaka minane, zaidi au michache ya hapo iliyopita, ni Clouds FM, East Africa Radio, Radio One, Magic, Uhuru FM na Times FM pekee ndizo zilizokuwa zikigombania mawimbi ya jiji la Dar. Bila kusahau vituo vya redio vya nje ya Dar hususan RFA na Kiss FM zote za Mwanza ambavyo navyo vimekuwa na sehemu yake kwenye soko la redio jijini humu pamoja na redio za dini.

Hata hivyo kadri mambo yanavyozidi kwenda mbele, ushindani umeendelea kuwa mkubwa sana. Hivi sasa kumeongezeka vituo viwili vya redio ambavyo ni EFM na Ghetto Radio iliyochukua nafasi ya Sibuka FM. Tayari EFM imeshaonesha cheche zake kwa kuwa redio inayosikilizwa kwa wingi na wananchi wa Dar.

Mkakati wake wa kuchukua watangazaji mashuhuri, umewafanya wamiliki wa redio zingine kuwa na wasiwasi wa kawaida kuwa huenda watangazaji wao tegemezi wanaweza kuchukuliwa. Tayari imeshafanya hivyo kwa kuchukua watangazaji mashuhuri wa michezo kutoka Radio One, Maulid Kitenge na Katanga, waliokuwa watangazaji wa Magic FM, Ssebo na Dizzo bila kumsahau mtangazaji wa zamani wa Times FM, Gadner G Habash.

Nayo Ghetto Radio ambayo makao yake makuu ni Kenya, inatarajia kuanza rasmi November 1 ikiwa tayari imechukua watangazaji mbalimbali kutoka Dar na mikoani. Nayo pia ina kila dalili kuwa italeta ushindani mkubwa.

Hatujasau pia kuwa kuna redio zingine zinazofanya vizuri Dar kama Capital FM, Choice FM na zingine ambazo nazo zinavutiwa wasikilizaji wengi. Katika kipindi cha miaka miwili mitatu ijayo, bila shaka kuna redio zingine mpya zitafunguliwa pia.

Maana yake ni kwamba, mwaka 2015 na kuendelea, redio hizi za Dar zitaingia kwenye ushindani mkubwa si tu katika kuhakikisha zinaandaa vipindi vya kuvutia, bali pia kuhakikisha vinawalipa vizuri watangazaji wake, lasivyo watachukuliwa na redio pinzani.

Pamoja na kuwa wasikilizaji wa redio huwa na mapenzi na kituo kimoja ama viwili ambavyo husikiliza mara kwa mara, wasikilizaji wengi ni watu wa kuhamahama. Msikilizaji huhama stesheni moja kwenda nyingine kutafuta kile anachopenda kusikiliza kwa muda huo.

Changamoto kubwa ni kumfanya msikilizaji aendelee kusikiliza kituo chako na asihame kwenda nyingine. Katika mazingira haya ambayo msikilizaji ana option nyingi, waandaji wa vipindi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wana ‘content’ ya maana inayomfanya msikilizaji asiwaze hata kuhamisha stesheni.

Hapo kwenye content ambapo hujumuisha maneno yanayozungumzwa na mtangazaji, muziki unaochezwa, habari zinazozungumzwa na mambo mengine, ndipo panapofanya stesheni moja kusikilizwa zaidi ya nyingine. Redio zenye waandaji wabunifu na waliopewa uhuru wa kutumia ubunifu wao ndizo zitakazoendelea kuongoza.

Kwa wasikilizaji, ushindani wa aina hii una faida kwao kwakuwa huwa na option ya kusikiliza vipindi vilivyo bora. Waswahili husema ‘vita vya panzi furaha ya kunguru’

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents