Habari

Sugu alia kwa uchungu bungeni akijibu tuhuma za ‘kumpora’ mtoto wake kutoka kwa Faiza

Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi aka Sugu amejikuta akilia kwa uchungu bungeni Ijumaa hii mara baada ya kutoa hoja binafsi kumjibu mbunge wa viti maalum wa Singida (CCM), Bi. Martha Mlata aliyemshutumu kwa kumpora mtoto wake Sasha kutoka kwa mama yake Faiza Ally waliyeachana na ambaye Mlata amemuita ‘Mnyonge.’

MR-II-SUGU-NA-MTOTO-WAKE
Sugu akiwa na mwanae Sasha

Sugu alipewa ruhusa ya kumchukua mwanae kutoka kwa Faiza kutoka na kushinda kesi mahakamani ya nani anastahili kuishi na mtoto huyo.

Akijibu shutuma za Bi. Mlata, Sugu alisema ameumizwa na kusikitishwa kwa suala lake la kifamilia kuingizwa ndani ya bunge na kuomba kuheshimiwa kwa masuala yake binafsi.

“Mheshimiwa naibu spika, kwa vile masuala haya binafsi mimi na mzazi mwenzangu na binti yetu, yameletwa hadharani mbele ya bunge tukufu, kwa vile masuala haya ni binafsi na ya kiunyumba yamevishwa joho la haki za wanawake na watoto na tuhuma nzito kutolewa juu yangu, mimi nalazimika kwa masikitiko makubwa na moyo mmzito kabisa kuyazungumzia hadharani mbele ya bunge lako tukufu,” alisema Sugu.

“Mheshimiwa naibu spika binti yangu Sasha Desteria anaishi Dar es Salaam na mama yake tangu alivyozaliwa tarehe 26 September 2012 na katika kipindi chote hicho mimi nimempelekea mama yake takriban shilingi 500,000 kwa mwezi kwaajili ya matunzo ya binti yetu kila mwezi. Aidha tangu awe na umri wa miaka miwili mimi nimemlipia Sasha ada yake ya shule takribani milioni 3 kila mwaka ambayo ni shilingi 750,000 kwa semester. Malipo haya ni nje ya fedha za nguo, chakula, vifaa vya kuchezea watoto pamoja na kulipia gharama za television za watoto ya cartoon katika kipindi chote tangu binti yangu alipozaliwa.

10852938_800529123337629_414595070_n
Faiza na Sasha

Mheshimiwa naibu spika, mzazi mwenzangu anayedaiwa kuwa mwanamke mnyonge na mheshimiwa Mlata, ni mwanamke anayejulikana katika kumbi za starehe karibu nchi nzima kwa kutokuwa na haya mbele ya hadhara wala mbele ya jamii. Ni mwanamke katika sherehe za tuzo za Kilimanjaro Music Awards zilizofanyika jijini Dar es salaam mwezi mmoja uliopita, alivalia nguo ambazo ziliacha sehemu zake za siri hadharani ili mpita njia azione. Picha zake katika mavazi hayo zilisambaa katika mitandao ya kijamii ya kuleta fedheha kubwa kwangu binafsi na bila shaka kwa watanzania wote wanaojali maadili katika masuala ya mavazi ya hadharani.

Kabla ya hapo picha zake nyingine wakati amevalia nepi ya mtoto yaani Diapers na kisha kusambaza katika mitandao ya kijamii. Kama angetaka mheshimiwa Mlata angeweza kupata taarifa hizi kabla ya kurusha tuhuma nzito ndani ya bunge tukufu,” alisisitiza Sugu.

Pia Sugu alizungumzia jinsi alivyolipeleka suala lake mahakamani mpaka mahakama kutoa uamuzi wa kutaka Faiza amkabidhi mtoto kwa Sugu.

“Mahakama ya mwanzo Manzese iliridhika na ushahidi wangu kwamba mzazi mwenzangu hakuwa na maadili yoyote ya kuweza kumlea mtoto wetu. Mahakama hiyo iliamuru kwamba binti yetu Sasha Desteria akabidhiwe kwangu ili niweze kumlea katika mazingira ya maadili ya usawa kwa mtoto na kwa umri wake. Hivyo mheshimiwa naibu spika kile ambacho kimedaiwa na mheshimiwa Mlata cha uporaji wa mtoto kiukweli ni amri halali ya mahakama ya Manzese iliyotolewa baada ya kusikiliza pande zote kuzingatia ushahidi uliotolewa.”

Hata hivyo Sugu alisema bado hajamchukua mtoto huyo kutoka kwa Faiza, na kwamba kuna uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya kifamilia kulimaliza suala hilo kwa amani.

Sugu pia amewataka wananchi kuheshimu mambo yake binafsi na kwamba shutuma zinazotupwa kwake hazistahili.

Baada ya kumaliza kutoka hoja hiyo, Sugu alionekana kulia kwa uchungu huku wabunge wenzake wakimliwaza. Naye naibu Spika, Job Ndugai, amesema hoja hiyo imefungwa bungeni.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents