Habari

Shule zapigwa marufuku kuwaondoa wanafunzi wasiofikia wastani wa ufaulu

Serikali imezitaka shule zote za msingi na sekondari binafsi zilizowafukuza ama kuwataka wazazi na walezi kuwahamishia watoto wao shule zingine kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kuwarudisha mara moja shuleni bila masharti yoyote.


Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nicolas Buretta kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambayo imeeleza kuwa wizara hiyo imebaini kuwepo kwa shule zisizo za serikali na hasa zinazomilikiwa na mashirika ya dini zilizokiuka utaratibu wa elimu nchini kwa kufanya matendo hayo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa shule hizo pia zimeendelea kukaririsha, kuhamisha shule nyingine darasa au kuwafukuza wanafunzi hao katika shule kwa kigezo hicho.

“Wazazi na walezi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu hizo, wahakikishe wanawarudisha watoto wao kwenye shule walizokuwa wakisoma ili waendelee na masomo kama kawaida,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha wizara hiyo imeendelea kuzitaka shule hizo kuwa na utaratibu wa kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo badala ya kukaririsha darasa kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule, na kwamba ikitokea ulazima wa kufanya hivyo taratibu zilizopo zifuatwe.

Wizara hiyo imeongeza kuzitaka shule zote zilizowataka wazazi na walezi kuwahamishia watoto wao katika shule nyingine kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu wa shule kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi hao bila masharti yoyote.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents