Habari

Serikali yawaondoa hofu wananchi juu ya hali ya upatikanaji chakula nchini

Waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi, Charles Tizeba amesisitiza kauli ya serikali kuwa Tanzania hakuna baa la njaa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.

Waziri Tizeba ameyaainisha hayo Jumatatu hii jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji na chakula nchini.

“Ndugu waandishi ukweli ni kwamba hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha sana katika maeneo mengi, hivyo siyo kweli kwamba kuna tatizo la njaa kama baadhi ya watu wanavyojaribu kupotosha,” alisisitiza Tizeba.

Pamoja na kusema hayo aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na chakula cha kutosha.

Aidha Tizeba alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imejipanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula ambapo hadi kufikia Januari 8 mwaka 2017 imenunua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea.

“Kati ya kiasi kilichonunuliwa, tani 38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima hivyo hadi kufikia tarehe 12 Januari, 2017 Wakala wana akiba ya tani 88,152.443 za mahindi.”

Jumatatu hii Waziri Mkuu Kassim majaliwa alikanusha kuwepo na baa la njaa nchini.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents