Habari

Serikali yaunda kikosi kazi cha kuzuia ‘viroba’

Serikali imeunda kikosi kazi cha Taifa cha kufuatilia pombe kali zinazofungashwa kwenye pakiti za plastiki maarufu kama ‘viroba’ zinazoingia mipakani kutoka nchi za nje.

Kikosi kazi hicho, mbali na kufuatilia pia kitakuwa na jukumu la kufanya ukaguzi na kitajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) , Uhamiaji na Polisi.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu hii mchana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, January Makamba amesema lengo la kuunda kikosi kazi hicho ni kudhibiti ‘viroba’ vinavyoingizwa nchini.

Amesema “Serikali imeunda kikosi kazi maalum cha kitaifa kwaajili ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa hatua hizi tulizozitangaza leo, kikosi hicho kinajumuisha watu kutoka ofisi ya Makamu wa rais, wizara ya mambo ya ndani ya nchi, wizara ya fedha na mipango, wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji, wizara ya afya, baraza la taifa la uhifadhi na usimamizi wa mazingira, mamlaka ya chakula na dawa, TBS,TRA, idara ya uhamiaji na jeshi la polisi, doria za ukaguzi kwaajili ya utekelezaji zitaanza wakati wowote kuanzia sasa.”

“Mtu yeyote atakayekamatwa katika doria hizo ambaye amekiuka masharti kwa masharti tuliyotangaza siku ya leo na hatua tulizotangaza siku ya leo kuanzia tarehe aliyoitangaza Waziri mkuu kuanzia tarehe 1 mwezi Machi atachukuliwa hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaokiuka.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema ifikapo Machi 1 mwaka huu, pombe hizo hazitaruhusiwa.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents