Habari

Serikali yatangaza neema mpya ya mikopo kwa Watanzania

WAZIRI wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk Juma Ngasongwa ametangaza neema mpya kwa kuwadhamini wajasiriamali ambao wanahitaji mikopo kutoka benki kupitia Mfuko wa Wwezeshaji wa Wananchi (MEF).

Na Patricia Kimelemeta

 

WAZIRI wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk Juma Ngasongwa ametangaza neema mpya kwa kuwadhamini wajasiriamali ambao wanahitaji mikopo kutoka benki kupitia Mfuko wa Wwezeshaji wa Wananchi (MEF).

 

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mfuko huo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Dk Ngasongwa alisema utawasaidia wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kwa kuwadhamini wanapohitaji kupata mikopo kutoka sehemu mbalimbali.

 

Alisema juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi katika kujikwamua kiuchumi ni za muda mrefu zinatokana na serikali kuona kuwa wananchi wengi wanahishi katika hali ngumu.

 

“Wananchi wengi wanaishi katika mazingira magumu, hivyo tumeamua kuanzisha mfuko huu kwa ajili ya kuwadhamini wananchi ambao wanahitaji kupata mikopo kutoka benki waweze kukopesha kwa masharti nafuu bila ya usumbufu kutoka mahali popote,'” alisema.

 

Aliongeza, lengo la uwezeshaji kwa wananchi juhudi za kukuza uchumi kama dira ya maendeleo ya Taifa ya kuhakikisha kuwa wanakuza soko la ajira ndani na nje ya nchi kutokana na wananchi wengi kukosa kazi kutokana na kuwa na elimu ndogo au kukosa ujuzi wa aina yoyote.

 

Alisema, lengo la kuanzishwa kwa mfuko huu ni kuikomboa nchi katika dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kupeleka kwenye uchumi wa kisasa wa uwezeshaji na maendeleo.

 

Alisema, mfuko huo pia utawashirikisha wananchi kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi wa uchumi na kutokomeza umaskini nchini na kutoa miongozo mbalimbali kuhusu uwezeshaji.

 

Ngasongwa alisema watanzania watapatiwa fursa ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuhimizwa juu utamaduni wa kuweka akiba na kukopa ili waweze kushiriki katika shughuli za uchumi endelevu.

 

Alisema mfuko huo pia utaainisha vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuutunisha, kuwawezesha na kusimamia miradi ambayo itakuza biashara zitakazoendeshwa na kumilikiwa na watanzania wenyewe.

 

Alisema jukumu lingine la mfuko huo ni kukuza uelewa pamoja na umilikaji sawa wa rasilimali na kuchangia nafasi za ajira kwa njia mbalimbali katika sekta za biashara, kilimo, ufugaji, viwanda utalii na madini.

 

Alisema mfuko huo utasaidia kuunganisha vikundi na taasisi mbalimbali zitakazoandikishwa chini ya Baraza la Uwezeshaji kwa mujibu wa sheria na kutoa huduma nyingine zitakazosaidia kuinua vikundi na kukuza uchumi.

 

Alisema dhamana ya mikopo itatolewa kulingana uwezo wa mfuko wenyewe na kwa masharti nafuu kwa ajili ya kuendesha miradi halali na ile inayoongeza thamani ya mali inayozalishwa, ikiwa mwananchi atashindwa kufuata taratibu hizo hawezi mikopo hiyo.

 

Alisema kuwa mikopo itaanzaia kiasi cha Sh50,000 hadi 500 milioni kwa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kulingana na biashara ya mtu au mtaji wake.

 

Ngasongwa alisema watendaji wa kata, tarafa na mikoa watawaelimisha wananchi juu ya upatikanaji wa mikopo hiyo ili waweze kufuata taratibu za kisheria.

 

Aliwaomba wamiliki wa makampuni makubwa, wafanyabashara na watu wenye uwezo ambao hawawezi kuchukua mikopo katika mfuko huu, kuchangia fedha kwa ajili ya kuuboresha ili uweze kuwanua wananchi wenye hali ya chini.

 

Mfuko huo una Sh 400 milioni ambazo zimetolewa na baraza katika kuanzisha mfuko huo ili uweze kujiendeleza.

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents