Habari

Serikali yapendekeza bajeti ya shilingi trilioni 31.6

Serikali imewasilisha bungeni mapendekezo yake ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2017/18 na ya kiasi cha Sh 31.6 trilioni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameyasema hayo Jumanne hii wakati akiwasilisha mapendekezo hayo bungeni mjini Dodoma.

Katika bajeti hiyo, fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka trilioni 11.8 mwaka 2016/17 hadi trilioni 11.9 mwaka 2017/18 sawa asilimia 38 ya bajeti yote.

Akiwasilisha mapendekezo hayo, Waziri Dkt Mpango ametaja baadhi ya maeneo ya kipaumbele kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, kuhuisha shirika la ndege Tanzania na shamba la kilimo na uzalishaji sukari la Mkulazi.

Aidha, Waziri Mpango ametaja changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017 hadi Februari mwaka huu kuwa ni mwamko mdogo wa kulipa kodi na hususani kuzingatia matumizi ya mashine ya kielektroniki.

Baadhi ya wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, nje ya ukumbi wa bunge wamesema serikali imechukua jitihada kubwa katika kuhakikisha inaondokana na utegemezi kuliko kutegemea fedha kutoka nje.

Wabunge bado wanaendelea na vikao na shughuli za utekelezaji katika kamati mbalimbali hadi Aprili 2 mwaka huu kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania April 4 mwaka huu mjini Dodoma.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents