Habari

Serikali yaanza mazungumzo ya kuwaokoa madereva 12 waliotekwa Kongo

Serikali imeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kuwaokoa madereva 12 wa malori kutoka Tanzania waliotekwa nchini Kongo (DRC) na kundi la waasi wa Mai Mai.
loritanzania

Waasi hao mbali na kuwateka madereva hao wametoa saa 24 kuanzia juzi saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, alisema waasi hao wametishia kuwaua mateka hao endapo hawatalipwa kiasi hicho cha fedha hadi kufikia jana saa 10 jioni.

Mindi alisema katika tukio hilo, madereva wawili wa Kitanzania walifanikiwa kutoroka na ndiyo waliosaidia kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.

“Serikali imepokea taarifa za kutekwa kwa malori 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jana (juzi) Septemba 14, 2016. Kati ya malori hayo manane yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Kitanzania, Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka Kenya.

“Kwa taarifa zilizopatikana watekaji ni kikundi cha waasi cha Mai Mai ambao baada ya kuyateka magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini na kisha kuteketeza kwa moto malori manne ambayo yote ni ya Dewji.

“Waasi hao wametoa saa 24 kuanzia jana saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia,” alisema Mindi.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeshachukua hatua za awali za kuwasiliana na Serikali ya DRC ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanaachiwa haraka iwezekanavyo wakiwa salama kabisa.

Alisema tukio la aina hiyo ni la pili kutokea ambapo katika mwaka jana masheikh kutoka Tanzania walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa Serikali hizo mbili juhudi ziliweza kuzaa matunda na masheikh hao kuachiwa huru bila madhara yoyote.

“Serikali ingependa kuushauri umma wa Watanzania hususan wafanyabiashara kuomba taarifa ya hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Kongo hususan Kivu ya Kusini kabla ya kusafiri kwenda maeneo hayo,” alisema Mindi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents