Habari

Serengeti Boys yakaribia kufuzu kombe la Mataifa ya Afrika – Vijana

Farid wa Serengeti Boys akichuana na Ondongo

TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kuichapa Congo Brazaville bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana mwakani.

Alikuwa ni mchezaji chipukizi Mudathiri Yahya aliyeifungia Serengeti Boys bao pekee katika dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza kwa mpira wa adhabu uliompita kipa wa Congo Brazaville, Ombandea Mpea katikati ya miguu ‘tobo’ na kujaa wavuni.

Kwa matokeo hayo sasa Serengeti Boys watalazimika kufanya kazi ya ziada kulinda ushindi wao huo watakapokuwa jijini Brazaville wiki mbili zijazo kwenye mchezo wa marudiano ili kukata tiketi ya kwenda Morocco.

Kocha Jacob Michelsen alisema mchezo ulikuwa mgumu kwa vijana wake, lakini anawashukuru kwa kupata ushindi huo.

“Nimefurahi tumeshinda ingawa ni ushindi mwembamba, sasa tunahitaji kujiandaa vizuri zaidi kwa ajili ya mechi ya marudiano,” alisema Michelsen.

Serengeti Boys sasa inahitaji ushindi au sare yoyote ili iweze kurudia rekodi yake ya mwaka 2003 walipokata tiketi ya kwenda Gambia, lakini waliondolewa kushiriki kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kubainika walitumia wachezaji waliozidi umri akiwamo Nurdin Bakari wa Yanga.

Katika mchezo wa jana, Congo walionekana kucheza kwa kujiamini na kutumia pasi fupifupi, lakini ngome ya Serengeti ilikuwa makini kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Katika dakika ya 14 mchezaji Seleman Bofu wa Serengeti Boys aliangushwa nje kidogo ya eneo la 18 na beki wa Congo hivyo mwamuzi Miiro Nsubuga kutoka Uganda alitoa adhabu iliyopigwa na Mudathiri na kwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa mashabiki wachache waliojitokeza uwanjani hapo.

Baada ya bao hilo, Congo waliamka na katika dakika ya 26 bado kidogo wangepata bao la kusawazisha baada ya mpira wa kona wa Ibara Vinny kuunganishwa kwa kichwa na Obassi Gambo na kupaa juu kidogo ya lango la Serengeti.

Katika dakika ya 32, mchezaji Hussein Ibrahim wa Serengeti Boys aliwatoka mabeki wa Congo na kupiga shuti lililodakwa na kipa Mpea.

Vijana wa Congo walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini washambuliaji wake walikosa mbinu za kuipenya ngome ya Serengeti Boys ambao wenyewe walikuwa wakicheza kwa kujihami na kutumia mipira mirefu na kushambulia kwa kushtukiza.

Kipindi cha pili vijana wa kocha Michelsen walirudi uwanjani kwa kasi zaidi na katika dakika ya 59 shuti la Mudathiri la umbali wa mita 35 lilitoka sentimita chache.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents