Habari

Sekondari za kata balaa

Shule za sekondari za kata, zinakabiliwa na matatizo lukuki ikiwemo uhaba wa vitabu, madarasa na walimu wa masomo ya sayansi.

Na Aneth Kagenda

 
Shule za sekondari za kata, zinakabiliwa na matatizo lukuki ikiwemo uhaba wa vitabu, madarasa na walimu wa masomo ya sayansi.

 

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika shule kadhaa za jijini Dar es Salaam hivi karibuni umebaini kuwa, shule nyingi zimefunguliwa zikiwa na upungufu mkubwa wa vifaa, walimu na vitabu.

 

Aidha, shule hizo hazina maabara ya kufundishia kwa
vitendo masomo ya sayansi.

 

Baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule hizo, wanadaiwa kuzikacha na kujiunga na shule za sekondari za binafsi.

 

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wanafunzi walikiri kuwepo kwa matatizo hayo katika shule zao.

 

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mugabe, Bw. John David, alisema wana upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na kuiomba serikali kulichukulia kwa umakini tatizo hilo.

 

Naye mwanafunzi Mwanaisha Hamza wa Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani, alisema kwa kipindi fulani, walianza masomo wakiwa wanakaa sakafuni lakini kwa sasa wamepata madawati.

 

Hata hivyo, alisema bado kuna upungufu wa vifaa vya maabara nzuri na maktaba yenye vitabu vya kutosha, jambo ambalo limewafanya wasome kwa shida.

 

Alisema licha ya kuanza masomo bila vitabu, pia mazingira ya kusomea sio bora kutokana na kukosa uzio, hali ambayo inasababisha watu kukatiza maeneo ya shule huku wengine wakiwa wanaongea kwa sauti za juu.

 

Katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa, baadhi ya shule zimebuni mpango wa kuwagawa wanafunzi katika mikondo ambapo baadhi wanaingia asubuhi na wengine mchana.

 

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mugabe, Bi.Theresia Herman aliiambia Nipashe kuwa shule yake ina matatizo mengi ambayo yanafanana na yale yaliyo katika shule nyingine.

 

Alisema kwa mfano, shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na tayari tatizo hilo limekwisha wasilishwa serikalini.

 

Akifafanua kuhusu upungufu wa walimu, alisema zaidi ya asilimia 90 ya walimu waliokuwepo shuleni hapo, wamejiunga na masomo katika vyuo vikuu mbalimbali na kusabisha pengo kubwa la walimu shuleni hapo.

 

“Nilikuwa na walimu wa kutosha, lakini asilimia 90 ya walimu hao wamekimbilia vyuoni kusoma kwa sababu wengi wao walikuwa na sifa za kuwafanya wajiunge na vyuo hivyo,“ alisema.

 

Kwa upande wa vitabu alisema havitoshi kwa kuwa wanafunzi 20 wanatumia kitabu kimoja.

 

“Kuna upungufu mkubwa wa vitabu shuleni hapa, hali ni mbaya kwa kweli, fikiri kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi 20, sasa hapo wataelewa kweli, nawaomba wazazi wajitokeze kuisaidia serikali kununua vitabu au wawanunulie watoto wao vitabu,“ alishauri.

 

Aliongeza kuwa, japo serikali imewapa Shilingi milioni tisa kwa kila shule, kunulilia vitabu, lakini kiasi hicho ni kidogo kupata idadi ya vitabu vitakavyotosheleza wanafunzi wake ambao ni zaidi ya 1,000.

 

Alisema wana umoja wa walimu wa shule za sekondari za kata Wilaya ya Kinondoni ambazo zipo zaidi ya shule 20 na wote wana matatizo yanayofanana.

 

“Tatizo utakalolikuta hapa kwangu na shule nyingine iwe Twiga, Kambagwa ama Goba ni hilo hilo sababu huwa tunakutana katika vikao mbalimbali vya wakuu wa shule hizo na vilio vyetu ni hivyo hivyo,“ alisema mwalimu huyo.

 

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Ilala Boma, Bi. Amra Ramadhan, alisema shule yake inakabiliwa na upungufu wa madawati.

 

“Madawati hamna na hili ni tatizo kubwa sana hasa katika kata kwa vile ukiwa unafundisha na wanafunzi wamekaa sakafuni inakuwa haileti picha mzuri,“ alisema.

 

Alisema pamoja na kukosa madawati pia kuna tatizo la upungufu wa walimu.

 

Alisema shule yake ina wanafunzi 901 wakati walimu ni 32 na walimu watatu wapo masomoni.

 

Kufuatia hali hiyo, aliiomba serikali kuongeza walimu katika shule yake na shule zingine kwa kuwa matatizo yao yanafanana.

 

Kuhusu vitabu, Bi. Amra alisema havitoshi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi alionao.

 

Aidha, aliishauri serikali kuongeza kwa wingi ajira za walimu ili kupunguza tatizo hilo.

 

Akizungumza na Nipashe kuhusu matatizo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Dickson Ndabise, alisema ujenzi wa shule hizo ulifanywa kisiasa zaidi.

 

Alisema matatizo yanayozikabili shule hizo hayawezi kutatuliwa kwa mara moja kama wengi wanavyofikiri, isipokuwa yatachukua muda mrefu.

 

Kuhusu walimu, alisema wizara haiwezi kufyatua walimu mara moja kama matofali bali ni lazima kuwe na mikakati ya kuwapata walimu wenye sifa zinazostahili.

 

“Ndio maana tulianzisha mpango wa kuwapata walimu wa leseni kwa miezi miwili maarufu kama `voda fasta` ili waweze kupata nadharia ya ualimu na kuendelea kuwafundisha wengine,“ alisema Bw. Ndabise.

 

Hata hivyo, aliongeza kuwa, malengo ya ujenzi wa shule za kata yalikuwa tofauti na yale ya Mpango wa Maendeleo kwa Shule za Sekondari Nchini (CEDEP).

 

Alisema CEDEP ilikuwa katika kipindi cha mpito ambapo ulianza tangu mwaka 2004 hadi 2009 ikiwa na lengo la kuandikisha wanafunzi asilimia 50 tofauti na ujenzi wa sasa wa kata uliofikisha asilimia 100 ya uandikishaji wanafunzi.

 

Bw. Ndabise, aliongeza kuwa, ili kukabiliana na matatizo hayo wizara ilifungua vyuo vingi vikuu kwa ajili ya kutoa elimu kwa walimu wengi ili kupunguza uhaba uliopo.

 

“Tumeweza kuandikisha walimu zaidi ya 500 katika vyuo vikuu vya elimu DUCE, Mkwawa na katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kupunguza uhaba huo ingawaje hatuwezi kutosheleza soko kwa mara moja kwani wapo walimu wengine wanaokimbia kazi hiyo na kwenda kufanya kazi nyingine,“ alisema.

 

Kuhusu vifaa alisema, matatizo yanayozikumba shule hizo sio ya wizara peke yake kwani ujenzi huo ulisimamiwa na halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya.

 

“Kama upo upungufu mwingine kila mdau ashiriki kuangalia sekta hiyo ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira yanayostahili,“ alisema.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents