Michezo

Salam za rambirambi alizotoa Jamal Malinzi kufutia kifo cha mwanahabari za michezo Amina Athumani

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kutokana na kifo cha Mwanahabari za michezo, Amina Athumani.

Katika salamu hizo ambazo pia zimekwenda kwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto; Rais Malinzi ameelezea kushtushwa kwake kwa taarifa za kifo cha ghafla cha Amina Athumani.

“Niseme tu wazi kuwa tangu kuanza kwa michuano ya mapinduzi, nimekuwa nikifuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanahabari. Huwa pia sikosi magazeti ya Uhuru na Mzalendo na kuona by line (jina la mwandishi) ya Amina. Mpaka matokeo ya fainali zilizofanyika Januari 13, mwaka huu.

“Sasa asubuhi hii ya januari 15 nimepata taarifa za kifo chake, ama kwa hakika zinasikitisha. Ni kifo cha ghafla, ninavyomfahamu binti huyo ni mchapakazi hodari, na mfano uko wazi kwani katika hali ya ujauzito alikuwa hakosi kufuatilia habari,” amesema Rais Malinzi.

Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu hizo za rambirambi kwa familia ya marehemu Amina Athumani, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.

“Binafsi naona ni kama askari Jeshi aliyefia vitani. Naweza kumwita ni shujaa, lakini ndiyo hivyo tena, huwezi kupingana na mipango ya Mungu, nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, naomba wenzangu pia muwe na subira wakati huu mgumu ambao tasnia na Kampuni ya Uhuru Publications imepoteza mwanahabari mahiri.

Taarifa zinasema Amina alifariki dunia Jumapili Januari 15, 2017 akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mnazimmoja, iliyoko Zanzibar mara baada ya kujifungua jana kwa mtoto ambaye pia alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Hadi mauti yanamkuta alikuwa Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo pamoja na gazeti la Burudani linalochapisha mahsusi habari za michezo na sanaa. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Amina Athumani mahala pema peponi.

Inna Lillah wa Innaa Ilaihi Rajaajiuun.

Sote wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents