Rais Mwinyi apigwa kofi jukwaani

Rais Mwinyi apigwa kofi jukwaani

Rais Mstaafu Rais Ali Hassan Mwinyi jana alipigwa kofi la shavuni na muumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Maulidi mara baada ya kuwataka Waislamu kujikinga na Ukimwi kwa kutumia kondomu kuliko kuwaambukiza watu gonjwa hilo hatari kwa jamii.

Rais Mwinyi ambaye pamoja na mambo mengine, alizungumzia masuala ya uchumi yanayoikumba nchi, alianza kuzungumzia vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa kusema kuwa zinaa katika Uislamu ni jambo haramu moja kwa moja.

Mwinyi aliendelea kudai kuwa mtu akifanya zinaa, kwa kutumia mpira (kondomu), atakuwa amefanya dhambi moja, lakini akifanya bila kutumia mpira, mtu huyo ni dalali wa kutembeza zinaa na Ukimwi.

Baada ya hapo akauliza mashekhe, kwamba kufanya dhambi Mungu anaweza akasamehe, lakini yule ambaye atafanya dhambi bila kondomu, bora ni vipi?

Mwinyi akaendelea kusema: “Dharura ya mtu asiyeweza kujizuia na kufanya zinaa, mashekh na maulamaa tufanyeje hapo?”

Baada ya kusema hivyo, akatoka muumini mmoja akapanda jukwaani na kumpiga Rais Mwinyi kofi upande wa shavu la kuume, akapepesuka almanusra aanguke na kuokolewa na maafisa usalama.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia kitendo hicho, kibao kilikuwa cha kushtukiza kwani kila mtu alidhani kijana huyo alikuwa anakwenda kumsalimia Kaimu Mufti Sheikh Suleyman Gorogosi aliyekuwa pembeni ya Mzee Mwinyi. Wengine walidhani kijana ni fundi mitambo na hivyo alikuwa anakwenda kurekebisha kipaza sauti.
Hali hiyo ilisababisha Mwinyi asitishe hotuba yake baada ya maafisa wa usalama na polisi kuvamia jukwaa na kumkamata mtuhumiwa aliyefanya kitendo kisicho cha kiuungwana.Katika harakati za kumkamata, askari hao walianza kumpiga na ukumbi ukapatwa na taharuki kubwa.

Baada ya kumdhibiti mtu huyo ambaye alitia dosari sherehe hizo zilizokuwa zimeandaliwa vizuri, wanausalama hao walimpakia kwenye gari na kuondoka naye.

Baadhi ya waumini walitaka kukimbia, wengine wakaenda kuwasaidia maafisa usalama kumkabili mtu huyo aliyempiga Rais Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa.

Kijana huyo ambaye ametambulika kwa jina la Ibrahim Said ana umri wa miaka 26.

 

Pole sana mzee wetu!

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents