Siasa

Raia wenye marungu `wawatimua` polisi

Wakazi wa eneo la mradi wa Luguruni Kibamba jijini Dar es Salaam, wamewazuia polisi na maafisa ardhi waliokwenda kupima eneo hilo ili kupisha ujenzi wa mji mpya.

Na Godfrey Monyo

 
Wakazi wa eneo la mradi wa Luguruni Kibamba jijini Dar es Salaam, wamewazuia polisi na maafisa ardhi waliokwenda kupima eneo hilo ili kupisha ujenzi wa mji mpya.

 

Nipashe ilishuhudia wakazi kadhaa wakiwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga, marungu na mawe kuwazuia kufanya kazi zao.

 

Maofisa hao walikwenda katika eneo hilo jana asubuhi ili kukamilisha vipimo na kisha wakabidhi eneo hilo kwa wafadhili ambao wanataka kujenga kituo cha hadhi ya wilaya.

 

Sambamba na maofisa hao kutimuliwa, pia walisema kuwa wamemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. John Magufuli kumjulisha hali ilivyo katika eneo lao.

 

Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mwenyekiti wa kile wanachoita Waathirika wa Uhamishwaji Kimabavu Luguruni na Kibamba Hospitali (WAKILUKI), Bi. Asma Sungura, alisema kamwe hawatakubali kuondoka katika ardhi hiyo kama haki haitafuatwa.

 

“Asubuhi nikiwa najiandaa kuwapeleka watoto shuleni mara niliwaona polisi wameambatana na maafisa ardhi ndipo nilipokwenda kuvaa bukta na kuwatimua mbio,“ alisema Bi. Sungura.

 

Alieleza kuwa akiwa pamoja na wananchi waliokuwa na mapanga, mawe na marungu waliwatimua mbio maafisa hao ambapo waliingia katika magari yao na kukimbilia kusikojulikana.

 

Alidai kuwa sio kwamba wanapinga kuhama katika eneo hilo ila utaratibu unaotumika kuwaondoa hapo sio wa haki.

 

Alitolea mfano wa mtu mwenye nyumba yenye thamani ya Sh. milioni 20 lakini anapewa fidia ya Sh. milioni saba na kutakiwa kuhama bila ya kupewa muda wa kutosha wala kuambiwa aende wapi.

 

“Sasa katika gharama kama hizi za ujenzi zinazopanda kila siku, mtu unapewa fedha kidogo namna hiyo, unadhani utaondoka vipi kwenda kuanza maisha mapya tena kwa kipindi kifupi?“ Alihoji Bi. Sungura.

 

Naye mwenyekiti wa kamati ndogo ya haki za waathirika wa mradi huo, Bw. Chrisant Kibogoyo, alisema kwa mujibu wa tangazo wanapaswa kuondoka ifikapo Januari 19 mwaka huu.

 

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa wao wanamiliki ardhi kihalali na kwa mujibu wa sheria za nchi na kwa kushirikiana na ngazi zote husika za serikali zikiwemo za serikali za vijiji, mitaa, kata, manispaa na wizara yenyewe.

 

Bw. Kibogoyo alisema ili mradi huo ufanikiwe, maafisa ardhi walitakiwa wahakikishe wanatenga raslimali za kutosha ili kuwapatia waathirika malipo ya fidia ya haki.

 

Aliongeza kuwa fidia hiyo inatakiwa ilingane na hali halisi itakayoweza kuwarejesha katika viwango vya maisha waliyokuwa nayo hapo awali kabla ya kuhamishwa.

 

Bw. Kibogoyo aliongeza kuwa inashangaza watumishi wa wizara na wale wa manispaa waliwalazimisha kuweka sahihi nyaraka mbalimabli zinazohusu mradi huo na kama wangekataa nyumba zao zingebomolewa bila malipo yo yote.

 

“Kutuhamisha kimabavu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Ardhi pamoja na Haki za Makazi kama zilivyoainishwa katika Sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, ambayo Tanzania imeridhia,“ alisema mwenyekiti huyo.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents