Pinda avalia njuga mapato ya jiji

Pinda avalia njuga mapato ya jiji
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amemwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya makusanyo ya
Stendi ya Mabasi Ubungo na kuwasilisha ripoti yake katika kipindi cha
mwezi mmoja


Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku nne katika Mkoa wa Dar es Salaam aliyoyafanya katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.

Sanjari na agizo hilo pia Waziri Mkuu alimtaka CAG kufanya pia ukaguzi katika Soko la Kariakoo ambalo alibainisha kwamba lina matatizo makubwa ya menejimenti.

Agizo hilo la Waziri Mkuu limetokana na kubaini kuwapo kwa upungufu katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi katika maeneo mbalimbali aliyotembelea ikiwamo Stendi ya Mabasi Ubungo.

Akizungumzia Soko la Kariakoo alisema soko hilo likisimamiwa vizuri ni chanzo kizuri cha mapato lakini hakuna usimamizi makini na kuwataka viongozi wa mkoa na manispaa kusimamia kwa makini masoko yote jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia hali ya masoko mengi hali yake sio nzuri ikiwa ni pamoja na kuwa mipangilio mibovu na kuhatarisha maisha ya watumiaji na katika kuchukua hatua katika baadhi ya masoko hayo ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Soko la Buguruni na Manispaa ya Ilala kuhakikisha hali ya mazingira inaboreshwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu umewashauri viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuangalia utaratibu wa masoko ya usiku kwa lengo la kuboresha huduma kwa wakazi na kuwapatiwa mapato.

Waziri Mkuu pia aliutaka uongozi wa jiji kufuatilia na kusimamia utaratibu wa magari madogo ya abiria (teksi) kuwa na rangi na kwamba utaratibu huo uliwekwa kwa sababu ya msingi ya usalama.

Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wakati wote wanasimamia uamuzi unaopitishwa na serikali na kuhakikisha unatekelezeka na kwamba anashangaa kuona utaratibu huo wa kupaka rangi kutosimamiwa kama inavyostahili.

Akizungumzia suala la usafi alisema serikali inaangalia uwezekano wa kuondoa ushuru katika magari na vyombo vya kuzolea taka na kutoa rai kwa kila manispaa kujiwekea utaratibu wa kununua vyombo viwili au vitatu vya taka kila mwaka ikiwa ni pamoja na magari, matrekta na matela.

Waziri Mkuu pia alitaka gesi itumike kukaangia samaki katika Soko la Samaki Feri badala ya kuni ambazo wingu la moshi wake unalichafua soko na mazingira.

Alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, mbele ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema kuhakikisha kuwa vibaka, wavuta bangi na wahalifu wengine walioko Soko la Samaki Feri katika eneo linaloitwa Lebanon, wanaondolewa mara moja.

Alisema pia kwamba hana hakika kama mabango yaliyozagaa jijini yanaingiza mapato ya kutosha kwenye halmashauri na kusema kuwa kazi ya ukusanyaji ushuru wa mabango ingebinafsishwa ili kuleta ufanisi.

Vilevile aliutaka uongozi wa Dar es Salaam kubuni njia ya kusaidia usafirishaji wa wanafunzi katika jiji ili kuwaondolea kero, hata ikibidi kutumia mabasi ya Kampuni ya Usafiri ya Dar es Salaam (UDA) ambayo Halmashauri ya Jiji ina hisa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents