Habari

Padri atiwa mbaroni akihusishwa na kifo

PADRI wa Kanisa Katoliki anayetuhumiwa kuhusika katika kumtoa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Dongobesh wilayani Mbulu, Veneranda Antony Amini, ambaye baadaye alipoteza maisha, ametiwa mbaroni.

na Richard Mwangulube, Arusha


PADRI wa Kanisa Katoliki anayetuhumiwa kuhusika katika kumtoa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Dongobesh wilayani Mbulu, Veneranda Antony Amini, ambaye baadaye alipoteza maisha, ametiwa mbaroni.


Habari zinaeleza kuwa, padri huyo, aliyekuwa akitafutwa kwa tuhuma za kumtelekeza mwanafunzi huyo baada ya kumsaidia kutoa mimba, alikamatwa akiwa mafichoni katika Parokia ya Mbulu.


Mwanafunzi huyo ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro, wiki mbili zilizopita na kuzikwa kijijini kwao Dongobesh, alifariki baada ya kutolewa mimba katika mazingira yasiyo safi na salama katika hospitali moja iliyoko Manyara.


Habari ambazo ziliandikwa na gazeti hili wiki iliyopita zinaeleza kuwa, vifaa vichafu vilivyotumika kumtoa mimba binti huyo, vilisababisha utumbo, mfuko wake wa uzazi na ubongo kuoza.


Hayo yalibainishwa kupitia uchunguzi uliofanywa na madaktari bingwa katika Hospitali ya KCMC, ambako mwanafunzi huyo alipelekwa na wazazi wake baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya, kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele.


Padri huyo aliyetajwa kwa jina la Stephen Uhuru, anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na mwanafunzi huyo, ambaye alijitambulisha kwa wazazi wake kuwa mfadhili wake kimasomo.


Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dongobesh, Mbulu, baba mzazi wa binti huyo, Mwalimu Anthony Yesaya Ammi, alithibitisha kukamatwa kwa padri huyo juzi, akiwa katika moja ya majengo ya Parokia ya Mbulu.


Akihojiwa kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Mbulu, Elias Goloi, alikiri kukamatwa kwa padri huyo na akasema, amekuwa akishikiliwa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi unaendelea.


Mkuu huyo wa wilaya aliwatoa hofu ndugu na jamaa za msichana aliyefariki dunia, baada ya kuwapo kwa uvumi kuwa, mtuhumiwa alikuwa akiandaliwa mpango wa kutoroshwa na jamaa zake, ambao wanataka kufanya hivyo kwa kisingizio cha kumuwekea dhamana.


Goloi alisema, suala linalohusu tukio hilo zima, hivi sasa liko katika uchunguzi mkali unaofanywa kwa kuhusisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama wilayani humo.


Alisisitiza kuwa, kwa hivi sasa, bado si rahisi kwa padri huyo kupata dhamana, hasa baada ya kuwapo kwa taarifa zinazoonyesha kuwa watu kadhaa wengine walihusika katika tukio zima la utoaji mimba wa mwanafunzi huyo.


“Wapo baadhi ya watu, ambao tunahisi wameshiriki katika tukio hili, ambao ni lazima uchunguzi wa kina ufanywe ili nao watiwe mbaroni,” alisisitiza.


Alisema kwamba, kumpa mwanafunzi mimba ni kosa kubwa na pia kumtoa mimba na kusababisha kifo ni kosa kubwa zaidi na serikali haiwezi kuyafumbia macho makosa makubwa kama hayo.


Ilielezwa awali na mmoja wa ndugu wa marehemu kuwa, padri huyo alifanikiwa kumrubuni binti huyo kwa njia ya kujifanya mfadhili wake, ambaye alikuwa akimgharimia masomo.


Padri huyo alijitokeza wakati Veneranda akijiunga na kidato cha kwanza mwaka 2006 katika Shule ya Sekondari Gidhim, iliyopo wilayani Mbulu.


Alibainisha kuwa, padri huyo aliamua kumhamisha na kumpeleka Shule ya Sekondari Endaraftal, iliyopo wilayani Karatu.


Alisema baada ya muda, walishangaa padri huyo akimhamisha tena binti huyo na kumpeleka Sekondari ya Dongobesh, ambako aliendelea kuwa na mahusiano naye kimapenzi.


Akisimulia zaidi, alisema walianza kuhisi uhusiano usiofaa baina ya binti yao na mfadhili wake, Aprili 20, mwaka huu, baada ya padri huyo, ambaye alihamishiwa Kiru akitokea Dongobesh, kufika kijijini Dongobesh na kuonekana akiwa na binti huyo.


Na baada ya kuulizwa, padri huyo alidai alifika hapo kumchukua ili akamnunulie vitu muhimu vya shuleni.


Aprili 26, binti huyo aliomba ruhusa kwa uongozi wa shule, kwa madai kuwa alikuwa anakwenda nyumbani kwa wazazi wake, ambako baba yake ni mwalimu katika Shule ya Msingi Dumanangw, na alipofika nyumbani, alipewa fedha na wazazi wake na kuaga kuwa anarejea shuleni.


Ndugu huyo, aliyejitambulisha kama shangazi wa marehemu, alisema hata hivyo, binti huyo hakufika shuleni tena na badala yake, alikwenda Babati, ambako inadaiwa alikutana na padri huyo, na walikwenda katika moja ya nyumba za kulala wageni mjini hapo.


Ilielezwa kwamba, baada ya siku kama mbili, padri huyo alimfikisha binti huyo katika hospitali moja (jina tunalo), iliyopo mjini Babati, akiwa mahututi. Baadaye, padri alimpigia simu mama mzazi wa binti huyo, ambaye kwa wakati huo alikuwa mjini Arusha.


“Baada ya kuona hali ya binti huyo ni mbaya, kabla hata ya wazazi wa binti huyo kufika, padri huyo anadaiwa kutoroka na kumwacha binti huyo katika hospitali hiyo, na baadaye alifika mama yake na baba yake, ambao walilazimika kumchukua na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi,” alisimulia shangazi huyo.


Uchunguzi uliofanywa na daktari katika Hospitali ya KCMC ulibaini kuwa, binti huyo alikuwa ametolewa mimba, lakini kitendo hicho hakikufanywa ipasavyo, kwani kulikuwa na uchafu uliokuwa umebaki tumboni na kufanya sehemu za mwili wake zianze kuoza.


Akisimulia mkasa huo kijijini kwake Dongobesh juzi, baba mzazi wa marehemu, Mwalimu Anthony, alisema: “Uchunguzi wa madaktari wa Hospitali ya KCMC umegundua kuwa, utumbo pamoja mfuko wa uzazi navyo vilianza kuoza.” Mwalimu Anthony alisema kutokana na hali hiyo, familia yake imeamua kufungua kesi polisi dhidi ya padri huyo.


Hata hivyo, alidai kuwa, uongozi wa kanisa jimboni Mbulu ulikuwa ukimkingia kifua padri huyo.


Mmoja wa madaktari walioufanyia uchunguzi mwili wa binti huyo, ambaye alikataa kutajwa kwa vile si msemaji wa hospitali hiyo, alisema binti huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi mitano, alikuwa ametolewa mimba kwa vifaa vichafu.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents