Habari

Ofisi ya Taifa ya Takwimu yakanusha taarifa ya ‘Sasa ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba’

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amekanusha taarifa ambayo ilizagaa katika mitandao ya kujamii kuwa Ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba.
takwimu_clip
Dkt. Albina Chuwa

Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo imesema, habari hizo zinatokana na taarifa iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo la tarehe 24 Juni, 2016, toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari “Sasa ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba”.

Imefafanua kwamba, Ukimwi hautapimwa nyumba kwa nyumba bali ofisi hiyo itafanya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania kuanzia Septemba 2016 ambapo Ukimwi utapimwa kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine nyingi ambazo hazitahusika moja kwa moja katika utafiti huu.

Utafiti huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na utahusisha watu wazima wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.

Aidha, katika utafiti huu kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia dawa hizo.

Hivyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa utafiti huu sio mpya katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa mwaka 2016 unafanyika nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents