Siasa

Ofisi ya Makamu wa Rais `kiti moto’

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, imeiweka `kiti moto` ofisi ya Makamu wa Rais, kuhusu matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za ofisi hiyo.

Na Mashaka Mgeta

 
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, imeiweka `kiti moto` ofisi ya Makamu wa Rais, kuhusu matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za ofisi hiyo.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. John Cheyo, aliwaambia waandishi wa habari jana, katika ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam kuwa, maofisa waliohusika katika mahojiano hayo, ni wahasibu katika ofisi ya Makamu wa Rais.

 

Bw. Cheyo ambaye pia Mbunge wa Bariadi Mashariki na Mwenyekiti UDP, alisema hatua hiyo ilifikiwa katika utaratibu wa kawaida wa kamati hiyo, kabla ya kufanyika kwa kikao cha Bunge mjini Dodoma, mwishoni mwa mwezi huu.

 

“Leo tupo hapa na tutapata taarifa kutoka kwa wahasibu kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo tutazungumzia hoja zilizopo mezani, tutawahoji itakapobidi ili kupata ufafanuzi kwa mambo yatakayojitokeza,“ alisema bila kufafanua.

 

Katika ofisi ndogo za Bunge, Nipashe ilishuhudia watumishi kadhaa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, miongoni mwao wakiwa na mjalada kabla ya kuingia katika chumba cha mkutano kinachotumika kwa ajili ya vikao hivyo.

 

Aidha, Bw. Cheyo, alisema kamati hiyo, haina uwezo wa kuhoji masuala yaliyojitokeza na kuapishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubaini ufisadi dhidi ya fedha za umma.

 

Taarifa hiyo iliyohusu ukaguzi uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya Ernst and Young, iliwasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick Utuoh.

 

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo iliainisha matumizi hewa yenye thamani ya takribani Sh. bilioni 133, yaliyofanywa kupitia Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA).

 

Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete, alitoa taarifa ya kukasirishwa na yaliyobainika katika ripoti hiyo, na kuchukua hatua kadhaa, ikiwamo kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Balali.

 

Bw. Cheyo, alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, tamko kama lililotolewa na Rais kuhusu ufisadi katika BoT, haliwezi kujadiliwa katika kamati za bunge, ikiwamo Kamati ya Hesabu za Serikali.

 

Bw. Cheyo alisema kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Bunge, ripoti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni katika kikao kitakachoanza mwishoni mwa mwezi huu mjini Dodoma.

 

Hata hivyo, Bw. Cheyo alisema uamuzi wa kuiwasilisha ripoti bungeni na njia itakayotumika, lipo chini ya mamlaka ya Spika wa Bunge.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents