ODM wapata Spika

MABISHANO makali yalizuka jana wakati Bunge lilipokutana kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya ambayo hatimaye yalikiwezesha chama cha upinzani nchini humo cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga kushinda kiti cha Spika wa Bunge.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


MABISHANO makali yalizuka jana wakati Bunge lilipokutana kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya ambayo hatimaye yalikiwezesha chama cha upinzani nchini humo cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga kushinda kiti cha Spika wa Bunge.


ODM ambao mgombea wao, Kenneth Marende alipata ushindi wa kura 105 dhidi ya 101 za mgombea aliyekuwa akiungwa mkono na chama tawala kwa namna yoyote ile utaendelea kuiweka serikali ya Rais Mwai Kibaki katika mazingira magumu kiutawala.


Awali kabla ya matokeo hayo, mabishano hayo yalitokana na mvutano baina ya kambi mbili; moja inayoongozwa na chama tawala cha PNU na ile ya upinzani chini ya ODM.


Kambi hizo zilianza kuvutana katika uchaguzi wa Spika. ODM, ambayo inalalamikia kuporwa ushindi katika kinyang’anyiro cha urais, ilikuwa ikiitaka nafasi ya Spika kwa udi na uvumba, ili kuhakikisha kuwa inaibana serikali kutekeleza masuala yake.


Katika mabishano hayo, mbunge wa upinzani, James Orengo, alitaka Spika achaguliwe kwa utaratibu wa kura za wazi. Wapinzani walilazimisha kura ya wazi wakidai kuwa kuna uwezekano wa kuiba kura iwapo itapigwa kura ya siri.


Hata hivyo, uchaguzi huo ulilazimika kuingia katika awamu ya pili na kisha ya tatu, baada ya wagombea kutoka kambi hizo kupata idadi ya kura inayokaribiana sana.


“Tulifanya uchaguzi mkuu kwa kura ya siri na mkaiba kura,” alidai mmoja wa viongozi wa ODM, William Ruto.


Kauli hiyo ilimlazimisha Waziri wa Sheria, Martha Karua kuingilia kati na kusema kuwa, kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa katika masuala kama hayo.


Hata hivyo, baada ya mabishano hayo, wabunge walianza kupiga kura ya siri, lakini wakitumia sanduku la kioo ambalo liliwekwa mbele ya Ukumbi wa Bunge.


Katika awamu ya pili, mgombea wa ODM, Marende, alipata kura 104 wakati mgombea wa PNU Francis ole Kaparo, akiambulia kura 102. Mgombea mwingine wa tatu aliyeishia raundi hiyo ya pili aliambulia kura mbili na hivyo kung’oka mapema.


Theluthi mbili ya idadi ya kura zlikuwa zikihitajika ili mtu ashinde nafasi hiyo katika raundi mbili za mwanzo na ya tatu mshindi hupita kwa ushindi wowote wa kura. Bunge hilo lina zaidi ya wabunge 210.


Awali, wabunge wa upinzani walikuwa wamepania kukaa katika viti wanavyopaswa kukaa wabunge wa serikali, lakini kiongozi wao, Raila Odinga, alikwenda kuketi katika kiti cha kiongozi wa upinzani bungeni.


Pia wabunge hao wa upinzani hawakusimama pale Rais Mwai Kibaki alipoingia bungeni kama ishara ya kutomtambua kiongozi huyo, ambaye ushindi wake tata ulizua vurugu, mauaji na uharibifu wa mali nchini kote.


Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Odinga na Kibaki kuwa katika chumba kimoja tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu Desemba 27, mwaka jana.


Ingawa vurugu zimetulia, lakini hali ya wasiwasi bado imetanda na jana kulikuwa na ulinzi mkali katika barabara nyingi mjini Nairobi, hasa katika maeneo karibu na jengo la Bunge.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents