Habari

NMB yawawezesha wateja wake kutuma pesa kwenda benki nyingine kupitia NMB Mobile

NMB imezindua rasmi huduma ya kuhamisha ama kutuma fedha (NMB Mobile T.I.S.S) kutoka katika akaunti za benki hiyo, kwenda kwenye akaunti za benki nyingine, sambamba na kufanya manunuzi na malipo. NMB Mobile T.I.S.S, ni huduma ya kwanza kutolewa na benki nchini Tanzania, ambayo imetajwa kuwa ni njia rahisi, salama na ya haraka katika mchakato wa kutuma ama kuhamisha fedha kutoka NMB kwenda benki nyingine.

Kaimu Meneja Mwandamizi wa Amana, Huduma za Bima na Huduma za Ziada katika Benki ya NMB, Stephen Adili akizungumza na wanahabari (Hawapo pichani)

Akizungumza katika hafla ya kuitambulisha huduma hiyo Adili alisema, Huduma hii inakuja kumaliza tatizo la wateja kutumia muda mwingi kwenye mchakato wa kuhamisha fedha. Muda ni mali na kwa kulitambua hilo, tumekuja na huduma hii ambayo inafanyika popote, hata ukiwa ufukweni unapunga upepo.”

Aliongeza ya kwamba, NMB Mobile T.I.S.S haiishii tu katika kuhamisha fedha kutoka akaunti ya NMB kwenda benki nyingine, bali inaenda mbali na kupokea ama kutuma miamala ya mitandao ya simu za mkononi. Huduma hiyo inayoweza kutumiwa na wateja wa NMB Mobile, inapatikana kwa mteja kubonyeza *150*66# kisha kufuata maelekezo.

Naye Geofrey Mwijage, ambaye ni Mkuu wa Uendeshaji wa shughuli za Kibenki wa NMB, alisema benki yake imejidhatiti vya kutosha katika kutanua huduma miongoni mwa wateja wao na Watanzania kwa ujumla. “NMB Mobile T.I.S.S inaenda kuwa mshirika sahihi wa Watanzania, katika kuharakisha maendeleo yao na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kuelekea Tanzania ya Viwanda,” alimalizia Godfrey.

Mbali na kuhamisha fedha unaweza kufanya mengi ukiwa na NMB Mobile ikiwemo kununua luku na muda wa muda wa maongezi wa mitandao tofauti nchini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents