Bongo5 Makala

Ni adhabu kali mno? Serikali yaipiga ‘stop’ Miss Tanzania, Sitti amponza Lundenga

Baada ya kudumu kwa kipindi cha miaka 20, serikali imeamua kulisimamisha shindano la Miss Tanzania kwa miaka miwili. Shindano hilo lililoanza tena mwaka 1994 (baada ya kuwa limesimama tangu mwaka 1967 ambapo Theresa Shayo alikuwa mtanzania wa kwanza kuvaa taji hilo) na Aina Maeda kuwa mshindi, lilikubwa na kashfa kubwa ya udanganyifu uliofanywa na Sitti Mtemvu.

IMG_50551-1

Mtemvu alidanganya umri wake hali iliyopelekea kuwepo na mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii ambako pia vielelezo halisi vya umri wake vilioneshwa. Kashfa hiyo ilipelekea serikali kuliagiza baraza la sanaa la taifa, BASATA kupewa kazi ya kufanya uchunguzi na kuja na maamuzi.

Hata hivyo wakati baraza hilo likiendelea kufanya uchunguzi wake kwa mwendo wa kobe, Sitti aliamua kujivua taji hilo mwenyewe. Nafasi yake ilichukuliwa na Lilian Kamazima aliyekuwa mshindi wa pili. Uamuzi huo wa Sitti ulionekana kama mwisho wa sakata hilo na kamati ya Miss Tanzania ikaamini kuwa inaweza ikaanza kupata usingizi.

Katika muda ambao kila mtu alikuwa amesahau kuwa BASATA ilikuwa haijatoa uamuzi wake, waandaji wa Miss Tanzania wamepata habari mbaya kwenye msimu wa Christmas. BASATA imelifungia shindano hilo kwa miaka miwili.

IMG_5031

Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza amedai kuwa uamuzi huo umekuja kutokana na malalamiko mengi dhidi ya shindano hilo. Mngereza alikiambia kituo cha runinga cha EATV kuwa imefika wakati waandaji warekebishe masuala kadhaa ili kuondoa malalamiko na manung’uniko miongoni mwa wadau ili kulipa heshima shindano hilo, pia liweze kuheshimika na kila mtu.

Mngereza alidai kuwa serikali kupitia wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imelipa dhamana baraza hilo kisheria kushughulikia masuala yote yanahusu sanaa na utamaduni hivyo baraza hilo lina mamlaka ya kuingilia kati endapo litajiridhisha kuwa kuna masuala hayaendi sawasawa.

Kuhusu masuala wanayotakiwa kuyarekebisha, Mngereza alisema kuna mambo mengi hayako sawa katika mchakato mzima kuanzia katika ngazi ya vitongoji, na baraza limekuwa likipata malalamiko karibu kila mwaka lakini kwa mwaka huu malalamiko yalikuwa mengi zaidi.

“Kama imefikia wakati hadi mshindi wa shindano mwenyewe analazimika kuvua taji lake kwa shinikizo, ina maana kuna tatizo, kwahiyo tumewapa muda ili wakaangalie upya mchakato mzima na wafanye marekebisho,” alisema.

Hiyo ina maana kuwa Lilian Kamazima aliyetwaa taji hilo baada ya Sitti Mtemvu kujivua, ataendelea kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia kwa mwaka 2015 kama ilivyopangwa, lakini hakutakuwa na mashindano mengine kwa kipindi cha miaka miwili ndani ya Tanzania kuanzia ngazi ya vitongoji.

Tuhesabu hasara ya uamuzi huo

Uamuzi wa kusitishwa kwa Miss Tanzania haujamkosesha ugali Hashim Lundenga tu bali watafutaji wengi nchini ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia mashindano ya Umiss kama sehemu ya kujipatia kipato. Kwa jinsi tulivyoielewa adhabu hiyo, ina maana kuwa, mwaka 2015 na 2016 hakutakuwa na shindano lolote la umiss, si Miss Sinza wala Miss Kinondoni, si Miss Nyamagana wala Miss Mwanza, si Miss Bukoba wa Miss Kagera!

Hasara haiishii kwa waandaaji tu, inarudi hadi kwa serikali yenyewe ambayo itapoteza mapato mengi yaliyokuwa yakitokana na upatikanaji wa vibali vya kuyaendeshea pamoja na kodi zingine. Wasanii wa muziki waliokuwa wakipewa mashavu ya kutumbuiza kwenye mashindano hayo nao hawatapata show hizi kwa kipindi cha miaka miwili. Pengine hasara kubwa zaidi ni Tanzania kutoshiriki Miss World kwa miaka miwili. Umeona jinsi uamuzi huo ulivyo na madhara makubwa?

Uamuzi umekuja muda mbaya?

Kuna sababu nyingi ya kwanini uamuzi huo mkubwa haujamake headlines kama ilivyopaswa kuwa. Kwanini iko hivyo? Simple – bad timing! Uamuzi huu umekuja muda mbaya na umechelewa sana. Uamuzi huu ulipaswa kuja mapema wakati issue ya Sitti Mtemvu ilikuwa bado ipo moto. Kipindi hicho watanzania wengi walikuwa wakitarajia kuisikia serikali ikitoa uamuzi mgumu kama huo kuonesha makucha yake.

Wananchi wamefurahi!

Ofcourse kwa sifa ambayo Miss Tanzania imejipajitia hivi karibuni, wananchi wengi wamefurahi. Siku za hivi karibuni, wananchi wamekuwa wakilichukulia shindano hilo kama la anasa tu linalowadhalilisha wanawake. Je huo ni mtazamo wa kweli? Hapana. Kinacholiponza shindano hilo kwa sasa ni ule usemi samaki mmoja akioza…. Miss Tanzania imetoa wasichana ambao kwa sasa alisimia kubwa wamefanya mambo makubwa na ni vioo vya jamii.

Adhabu hiyo ni sahihi?

Kwa haraka haraka wengi wanaona adhabu hii ni sahihi. Lakini ukiangalia madhara yake, hii ni adhabu kali mno. Kwakuwa chanzo kikubwa cha adhabu hii ni sakata la Sitti Mtemvu, kasoro kubwa ipo kwenye ngazi ya juu ya kamati ya Miss Tanzania. Mtu pekee aliyetakiwa kupewa adhabu ni Hashim Lundenga ambaye kampuni yake ya Lino Agency ndio inayolisimamia katika katika ngazi ya mwisho.

Serikali ilitakuwa kumsimamisha yeye na kutangaza tenda kwa makampuni mengine ambayo yangelisimamia. BASATA ingechangua kampuni itakayofaa ambayo ingepewa masharti na vigezo vinavyohitajika. Kasoro kubwa ilikuwa kwa Lundega ambaye alikuwa ameanza kuliendesha shindano hilo kimazoea na wengi walikuwa wanapendekeza umefika wakati sasa watu wengine wachukue usukani. Lasivyo hakutakuwa na mabadiliko yoyote kama miaka miwili ikiisha na shindano kuendelea kuendeshwa na sura zile zile.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents