Siasa

Mwanasheria mkuu asema hajui lolote kuhusu Ballali

TIMU ya Rais ya Kuchambua Taarifa ya Ukaguzi wa tuhuma za upotevu wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema haijui lolote juu ya aliyekuwa Gavana wa benki hiyo, Daudi Ballali kuhusika katika upotevu wa fedha hizo kwa kuwa haijapata ushahidi wa kuhusika kwake.

Na Muhibu Said

 

 

 

TIMU ya Rais ya Kuchambua Taarifa ya Ukaguzi wa tuhuma za upotevu wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema haijui lolote juu ya aliyekuwa Gavana wa benki hiyo, Daudi Ballali kuhusika katika upotevu wa fedha hizo kwa kuwa haijapata ushahidi wa kuhusika kwake.

 

 

 

Kauli hiyo ambayo ni ya kwanza kutolewa tangu timu hiyo ianze kazi yake siku chache zilizopita, ilitolewa na Mwenyekiti wake, Johnson Mwanyika alipotakiwa na mwandishi wa Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, kueleza iwapo Ballali atarejeshwa nchini kujibu tuhuma za upotevu wa fedha hizo katika akaunti hiyo au la.

 

 

 

Ballali ambaye aliondoka nchini katikati ya mwaka jana kwenda kutibiwa nchini Marekani na kuacha maswali kwa wengi hadi sasa juu ya hospitali anayotibiwa nchini humo, alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete baada ya ripoti ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young, kubaini upotevu wa zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.

 

 

 

Mwanyika ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema hawezi kuzungumzia lolote kuhusu kurejeshwa kwa Ballali nchini kujibu upotevu wa fedha hizo au la kwa kuwa hajui lolote, kuanzia kuondoka kwake nchini wala kulazwa kwake hospitali nchini Marekani.

 

 

 

“Mimi sijui lolote kuhusu Ballali. Kwani mimi ndiye niliyemuondoa hapa nchini au ndiye niliyempeleka kulazwa hospitali huko Marekani?” alihoji Mwanyika.

 

 

 

Alisema kazi pekee aliyopewa na rais kupitia timu hiyo, ni kupeleleza, hivyo, kamwe hawezi kuzungumzia lolote kuhusu Ballali na kusema kwamba wanaopaswa kuulizwa lolote kuhusu gavana huyo wa zamani wa BoT, ni uongozi wa benki hiyo.

 

 

 

Mbali na hilo, alisema hatua ya Rais Kikwete kumfukuza kazi Ballali ni ya utekelezaji wa taratibu za serikali za uwajibishaji wa viongozi wa umma yanapobainika matatizo katika taasisi wanazoziongoza na wala haijamaanisha kuwa amehusika katika upotevu wa fedha hizo.

 

 

 

Hata hivyo, alisema upelelezi unaofanywa na timu yake kuhusu taarifa ya ukaguzi huo, ndio utakaotoa majibu iwapo Ballali alihusika katika upotevu wa fedha hizo au la na kwamba, iwapo watapata ushahidi wa kutosha kwamba, alihusika watachukua hatua zinazohusika.

 

 

 

Timu hiyo inaundwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea na Naibu wake, Lilian Mashaka.

 

 

 

“Itategemea upelelezi wetu. Tukipata ushahidi wa kutosha unaomhusisha na upotevu wa fedha hizo, tutachukua hatua,” alisema Mwanyika.

 

 

 

Aliwataka wananchi kuwa na subira na kuendelea kutoa ushirikiano kwa timu yake ili kuhakikisha ukweli unajulikana na kuwekwa hadharani kwa maslahi ya taifa.

 

 

 

Ballali aliachishwa kazi na Rais Kikwete mwanzoni mwa mwezi huu baada ya ukaguzi wa EPA kubaini kupotea kwa mabilioni ya shilingi katika akaunti hiyo.

 

 

 

Hata hivyo, wakati rais anatengua mkataba wake, Ballali alikuwa tayari yuko nchini Marekani alilikokwenda mwishon mwa Agosti mwaka jana kwa ajili ya matibabu.

 

 

 

Mpaka sasa haijulikani aliko ingawa kuna taarifa za kutatatisha zinazodai kuwa yuko Marekani na nyingine zinadai kuwa alitorokea kwenye visiwa vya Malta.

 

 

 

Awali ubalozi wa Marekani nchini ulisema hawajui kama yuko huko lakini baadaye walisema bado yuko nchini humo.

 

 

 

Hivi karibuni iliyopitia Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa alidai kuwa Ballali katoroshewa kwenye visiwa vya Malta.

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents