Habari

Muungano wa wapinzani ni ‘usanii’-Mtikila

MWENYEKITI wa Democratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila ameuita muungano wa vyama vya upiunzani nchini ‘usanii’ unaolenga kuvuruga vuguvugu la upinzani nchini.

Na Mwandishi Wa Majira


MWENYEKITI wa Democratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila ameuita muungano wa vyama vya upiunzani nchini ‘usanii’ unaolenga kuvuruga vuguvugu la upinzani nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ilala, Mchikichini jana Mchungaji Mtikila alisema ‘usanii’ huo unadhihirishwa na baadhi ya vikao alivyokaa na viongozi wenzake hao wa upinzani kwa lengo hilo hilo la kuunganisha vyama.


Mchungaji Mtikila alisema Agosti mwaka 2003 walifanya kikao cha pamoja na Mwenyekiti wa TLP Bw. Augustino Mrema na NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia kuzungumzia njia ambazo wangezitumia kuungana lakini hakikufanikiwa.


Miongoni mwa majadiliano yao yalikuwa kutaka kuwepo kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kupinga uuzaji holela wa mashirika ya umma, na kutetea haki za wazawa.


Baada ya kikao hicho walikubaliana kuunda kamati ya makatibu wakuu wa vyama vya upinzani kuandaa mkataba ambao vyama vyote vingesaini kama ishara ya makubaliano ya pamoja.


Mchungaji Mtikila alidai kwamba siku ya kuweka saini alishangaa kuona CCM imekaribishwa na Katibu Mkuu alialikwa kama mgeni wa heshima.


“Niliishiwa nguvu kuona mgeni wa heshima akisalimia kwa salamu maalumu na kusema..umoja, na wenzangu wakaitikia ..ni nguvu na kwa umoja tutashinda,” salamu ambayo alidai kutoifahamu ilitungwa lini na kuongeza kwamba makubaliano yalipoletwa kwa ajili ya kuweka saini yalikuwa yamebadilishwa vipengele walivyovijadili na kumlazimu kukataa kuweka saini.


Aprili mwaka 2004 vyama vyote 18 viliitwa Dodoma kwa ajili ya kujadili masuala ya uchaguzi yakiwepo kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi na kuanzishwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo Mchungaji Mtikila anadai kwamba walifikia makubaliano ambayo vyama vyote waliweka saini.


Miezi miwili baada ya mkutano wa Dodoma kwa mujibu walikutana tena Dar es Salaam ambapo walikubaliana kukataa utaratibu uliokuwa unatumika kuandaa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kukataa kujadiliana na Tume ya Uchaguzi kwa kuwa waliweka saini makubaliano ya kuikataa huko Dodoma.


Utaratibu walioukataa na kila chama kuweka saini ni kuiruhusu Tume ya Uchaguzi kuandaa daftari hilo kwa kutumia watumishi wa Serikali inayoongozwa na CCM pamoja na matumizi ya Jeshi la Polisi wakati wa kuandaa daftari hilo na wakati wa uchaguzi.


Katika kikao hicho cha Dar es Salaam ambacho Mchungaji Mtikila alisema kiliitishwa na Tume ya Uchaguzi, walikubaliana kuhudhuria na kuondoka bila kujadili ili waiache tume na watumishi wake peke yao.


“Nilitangulia kuondoka nikidhani wenzangu watanifuata, ajabu baada ya siku chache nasikia Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF na Dkt. Wilbrod Slaa wa CHADEMA wakilaani viongozi wa upinzani waliotoka nje ya mkutano jambo tulilokuwa tumekubaliana,” alielezea Mchungaji Mtikila.


Baada ya kuona tamko la CHADEMA na CUF Mchungaji Mtikila anadai kwamba aliwaita viongozi wote wa upinzani wakiwepo Prof. Lipumba na Dkt. Slaa kwenye mkutano mwingine ambao ulikuwa na madai yale yale lakini kwa kupitia mahakamani.


Vikao vingine walivyokuta ambavyo vingeweza kuunda muungano huo ni pamoja na safari ya viongozi kumi wa upinzani nchini Ufini ambapo viongozi aliofuatana nao wakiwemo Prof. Lipumba na Dkt. Slaa walikuwa wakisifia amani, juhudi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Serikali na kuacha mambo ya msingi.


Baada ya kuona wenzake wanatoa sifa za nchi tu aliamua kuongelea mambo ya rushwa ambayo yalikuwepo kwenye Ripoti ya Kimataifa ya Amnesty International ambapo baadae alipewa heshima ya kula chakula cha jioni na Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambayo kwa mujibu wa Mchungaji Mtikila inaongoza duniani kwa kutokuwa na rushwa.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents