Burudani

Mitandao ya kijamii ni mtaji wenye thamani kubwa kwa wasanii na mastaa

Miaka mitano iliyopita, ili msanii afikishe ujumbe kwa mashabiki wake, ilimlazimu kuhojiwa kwanza kwenye vyombo vya habari. Redio, TV na magazeti ndio zilikuwa njia pekee za kufikisha ujumbe wao.

social-networks-masthead.20131010231035

Lakini sasa mambo yamebadilika kabisa. Uamuzi wa kusambaza ujumbe wa msanii kwa umma upo kwenye kiganja chake mwenyewe. Kuanzishwa na kukua kwa mitandao ya kijamii, kumerahisisha mawasiliano ya watu duniani kote na wasanii hawajaachwa nyuma na maendeleo hayo.

Mitandao ya kijamii hususan Facebook, Twitter na Instagram imegeuka kuwa majukwaa muhimu wanayotumia wasanii wote duniani kuwasiliana na mashabiki wao, kutangaza kazi zao kama vile nyimbo, album, kanda zao mseto au ujio wa video zao. Wengi wamekuwa wakitumia mitandao hiyo kuweka picha zinazoonesha wakati wakitumbuiza kwenye show zao ama wakati wakitengeneza video zao mpya.

Mitandao hiyo imekuwa ikitumiwa sana na vyombo vya habari kupata habari za wasanii bila hata kuwahoji ama kuwapigia simu. Kwa kiasi kikubwa sasa, mitandao hiyo imekuwa sehemu muhimu ya vitu anavyovihitaji msanii katika zake.

Leo hii Diamond Platnumz ana likes zaidi ya 452,773 kwenye Facebook, followers zaidi ya 261,000 na zaidi ya 124,000 kwenye Twitter. Hiyo ina maana kuwa akiandika post moja kwenye mitandao hiyo, inawafikia zaidi ya watu 837,773 kwa wakati mmoja. Hiyo ni zaidi hata namna ambavyo ujumbe ama tangazo husikilizwa kwenye redio au TV au kusomwa kwenye gazeti.

Msanii anapotumia Twitter au Instagram inampa nafasi ya kuongea na mashabiki wake ambao mara nyingi hawana mawasiliano naye ya karibu kama namba ya simu, lakini wanahamu ya kuwasiliana naye.

Kutokana na pressure ya kuzifanya akaunti zao kuwa active mara nyingi, wakati mwingine msanii anatakiwa kuwa makini kwa kile anachokiandika hasa pale anapokuwa hana jambo la msingi kuandika. Kwakuwa akaunti nyingi za wasanii wa Tanzania hususan zile za Instagram hutumiwa na wasanii wenyewe na sio mtu ama watu wanaosimamia, msanii anapaswa kuwa makini zaidi kwakuwa mawasiliano ya umma ni fani ambazo watu wamesoma vyuoni.

Kutokana na ukweli huo ndio maana mastaa wakubwa duniani huajiri timu ya watu maalum ambayo humsaidia kuweka vitu vyake japo wakati mwingi pia msanii huandika mwenyewe. Kuna matukio mengi yamewahi kutokea kwa Tanzania ambapo msanii hujikuta akikosolewa vikali kwa picha au maneno aliyoandika. Mastaa kibao wamejikuta wakitukanwa matusi ya nguoni kwa post zao ambazo wasomaji huona zinawakwaza.

Wakati mwingine sio rahisi kuepukanana followers ambao huamua kumtukana msanii kwa makusudi na tumeshuhudia. Wapo mastaa kibao ambao wamewahi kurushiana matusi na shabiki. Wema Sepetu, Diamond Platnumz, Ommy Dimpoz na Kajala Masanja ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakipokea matusi kutoka kwa mashabiki wenye hasira kwa kile walichokiandika ama tu kutokana na jinsi wanavyowachukulia.

Pamoja na hivyo, mitandao ya kijamii haiepukiki na msanii anaiihitaji mno bila kuzingatia maoni ya followers wengine wenye chuki. Tweets za kila siku, kuweka status Facebook ama picha akiwa studio, humfanya msanii awe karibu na jicho la umma kila siku.

Wasanii wengi wanatakiwa kutumia mitandao mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wanampata kila shabiki hata wale ambao hawatumii Instagram au Twitter lakini Facebook wapo. Wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaipa mitandao yote uzito sawa na sio kuupendelea mtandao mmoja. Utafiti unaonesha kuwa wasanii wengi wa Tanzania wanatumia zaidi Instagram kwa sasa lakini wanasahau kuwa Facebook ina watumiaji wengi zaidi.

Mitandao ya kijamii inawasaidia wasanii kuendelea kuwepo midomoni mwa watu hata kama hawana kazi mpya redioni. Ni tofauti na zamani ambapo ilihitajika msanii kuwa na kitu kipya ili watu wamzungumzie. Msanii kama Diamond ameendelea kuwa kwenye vichwa vya habari kila siku kwakuwa amekuwa akiitumia vyema mitandao ya kijamii kutangaza mambo yake.

Mitandao ya kijamii inatumiwa na wasanii kama sehemu ya kurekebisha mambo yanapokuwa yameenda tofauti. Kwa mfano wasanii wengi wamekuwa wakitumia Facebook na Instagram kutoa ufafanuzi wa jambo lililoandikwa kwenye magazeti ya udaku hasa linapokuwa la uongo.

Pale msanii anapokosea kitu, hutumia pia mitandao hiyo kuomba radhi. Mashabiki huwapenda wasanii wanyenyekevu. Kwakuwa huhitaji kifua kipana kuomba msamaha, mashabiki huvutiwa na wale wenye uwezo wa kufanya hivyo. Mfano mzuri ni jinsi Diamond alivyowaomba radhi mashabiki wake wa Ujerumani baada ya show kutofanyika.

Wasanii wao wenyewe ni brand. Diamond, Alikiba, Mwana FA, Wema Sepetu, Kajala na wengine wote hao ni brand. Iwe wanafanya muziki, wanafanya filamu, wanamichezo, mastaa sio tu watu wa kawaida. Lakini wanafanya mambo mengine ambayo huwapa fedha pia. Wapo wenye maduka ya nguo na biashara zingine na hivyo Twitter, Facebook, na Instagram kuzitangaza kwa mashabiki wao.

Mitandao ya kijamii ni hazina ambayo kila msanii anaweza kuwa nayo na ikamsaidia katika maisha yake. Wasanii wanachotakiwa kufanya ni kuitumia vizuri kujiongezea mashabiki na sio kujipunguzia mashabiki.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents